Chama cha watu wenye ulemavu wa Viungo Zanzibar wamefunga mafunzo maalum ya mchezo wa mpira wa wavu wa kukaa (Volleball siting) kwa watu wenye ulemavu Zanzibar yaliyofanyika kwenye viwanja vya Amani mjini Unguja.

Akizugumza na Zanzibar24 Hassan Haji Silima  Mwenyekiti wa michezo kwa watu wenye ulemavu wa Viungo Zanzibar amesema mafunzo hayo yana lengo la kuwapa mafunzo viongozi wa watu wenye ulemavu wa viungo  kutoka mawilayani ili kuhakikisha mchezo huo unachezwa kwenye kila wilaya.

Kwa upande mwengine Hassan amesema bado kwa kuwa mchezo huo ni mpya ila wanaamini iko siku watakuja kuuelewa zaidi kwa kuwa mafunzo hayo yalikuwa ni ya vitendo na darasani hivyo watapiga hatua na kuusambaza mchezo huo na kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.

“Bado kuna changamoto ya viwanja, kwa Zanzibar mchezo huu unatakiwa uchezwe ndani na uwanja unatakiwa uwe na taizi ili uteleze ila sisi tutafanya jitihada na ya kuishawishi serikali ili kuona tunatengewa japo viwanja viwili kwa unguja na Pemba “ Alisema Hassan.

Hata hivyo Hassan amesema jumla ya wilaya saba tu ambazo hucheza mchezo huu kwa unguja na Pemba kwa hivyo bado kuna changamoto kwa walemavu wengi kutoshiriki michezo na wanahitaji kuwezeshwa ili kuona mchezo huo unakuwa sehemu ya michezo inayoitangaza Zanzibar kimataifa na kitaifa.

“Tunamshukuru mwakilishi wa jimbo la Chumbuni ametuahidi kwenye sherehe za mapinduzi zinazokuja kuhakikisha tutaonyesha mchezo huu mbele ya hadhara za watu kwenye kilele cha sherehe ili kupata nafasi kwa baadhi ya watu wenye ulemavu wa viungo kushawishika na mchezo huu” Alisema Hassan Silima.

Aidha ametoa wito kwa jamii kufahamu umuhimu wa michezo kwa watu wenye ulemavu wa Viungo Zanzibar kwa kuwa michezo hiyo huchezwa kimataifa kwa sasa na kutaka wadau wa michezo kukiunga mkono chama cha chao kwa kuwa kina malengo ya kuitangaza Zanzibar kwenye mchezo huu.