ENEO lenye historia kubwa barani Afrika la Mkamandume Wilaya ya Chake Chake Pemba, ambalo kwa sasa linafanyiwa matengenezo makubwa, limeanza kuvuta hisia za wananchi na wageni wengine, baada ya kuripotiwa kufukuliwa kwa Kisima wivu.

Taarifa zinaeleza kuwa, wakati huu wa matengenezo ya eneo hilo, moja ya jambo kubwa ambalo limewavutia wananchi ni pamoja na kufukuliwa kwa kisima hicho, ambapo kinasemakana kikitumiwa na wanawake wawili bila ya kuonana.

Akizungumza na mwandishi wa pembatoday, Mratibu wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale Pemba, Khamis Ali Juma, alisema, tayari wananchi wamekuwa wakionekana kwa wingi eneo hilo.

Alieleza kutokana na historia ya Mkamandume, kuvuta hisia za wananchi mbali mbali na hata wageni wengine, ndio maana pamoja na kwamba matengenezo yanaendelea, lakini idadi ya wananchi wanaokwenda kushuhudia kisima hicho inaongezeka.

“Ni kweli ingawa kwa sasa Serikali kupitia wizara yake ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale, wanalifanyia matengenezo eneo la Mkamandume, lakini baada ya kuwepo kwa taarifa ya kuonekana Kisima wivu sasa wananchi wamejaa,’’alifafanua.

Aidha Mratibu huyo alisema matengenezo ya eneo hilo la Mkamandume yenye lengo la kurejesha uasili wake, linaweza kufungua milango mipya ya utalii kisiwani Pemba.

Alieleza kuwa, tayari kuta tatu na mtaro aliokuwa akiutumia mfalme wa Mkamandume kuingia kwenye makaazi yake, umeshapatikana na umejaa maji kama ilivyokuwa asili.

Mratibu huyo alisema, baada ya mtaro huo kuonekana sasa kinachofuata ni matengenezo tu, ili uwe kama ule aliokuwa akiutumia Mkamandume mwenyewe.

“Kama historia ilivyo pale, kwamba mfalme alikuwa akiingia kwa mashua maamlum kutoka baharini hadi ndani ya makaazi yake kwa kutumia mtaro, laki ni kwa karne ulikuwa umejifukia lakini sasa umeshafukuliwa,”alifafanua.

Alisema baada ya kupatikana kwa kisima hicho, sasa kazi inayofanywa na wataalamu wao ni kuzifanyia matengenezo ngazi zote mbili zilizokuwa zikitumiwa na wake wa Mkamandume.

Baadhi ya wananchi wa Pujini wanaoisi karibu na eneo hilo la kihistoria, waliishauri Idara ya Makumbusho pindi kazi hiyo itakapokamilika, wawakumbuke kwa ajira za kudumu.

Walisema, wao wamekuwa walinzi wakubwa wa eneo hilo tokea wizara husika haijalitangaaza kama eneo la kihistoria, sasa ni vyema, kazi ikimalizika la matengenezo waangaliwe kwa kupatiwa ajira.

Ali Khamis Omar na Asha Haji Mussa ambao wamemaliza masomo yao ya kidato cha sita, walisema wapo wenzao ambao wanasifa za kuwepo eneo hilo, hivyo ni vyema wakapewa kipaumbele cha kwanza.

Mwanzoni mwa mwezi April mwaka huu, Kamati ya wajumbe wa baraza la wawakilishi ilipotembelea, ilipongeza hatua iliofikiwa ya matengenezo katika eneo hilo la Mkamandume.

Matengenezo ya eneo la kihistoria la Mkamandume yalianza mwishoni mwa mwezi Mach mwaka huu, ambapo kazi hiyo kwa awamu ya kwanza, itakamilika mwaka mmoja na nusu.

Zaidi ya shilingi milioni 400 zinaendelea kutumika katika awamu ya kwanza ya matengenezo ya eneo la kihistoria la Mkamandume ,lililopo Pujini wilaya ya Chake chake, kazi inayofanywa na Kampuni ya Shmanjo ya Kisiwani Pemba.

Inasemekana Wareno walikuwa wa kwanza kukikalia kisiwa cha Pemba kwa mabavu, pale wakaazi wake wa asili, yaani wapemba wa kale, walipotimuliwa na Imam Sultan bin Seif, mnamo mwaka 1652.

Na kuanzia hapo, kisiwa hicho pamoja na kile cha Unguja vikawa chini ya “Milki ya Sultan wa Oman”, ingawa mwaka 1711, mjukuu wa Seif bin Sultan aliachia ngazi baada ya kupoteza udhibiti wa kuendesha dola na mahala pake kushikiliwa na ukoo wa Al’Busaid. Ma – sultani wa ukoo wa Al’Busaid ndio waliokuja kuwa masultan wa Zanzibar kwa miaka kadhaa baadae.

Seyyid Said bin Sultan bin Ahmed , ambae alitawala kati ya mwaka 1804  hadi mwaka 1856, alikuwa ni mjukuu wa Ahmed bin Said, kiongozi wa kwanza wa ukoo wa Al’Busaid, alienyakuwa Usultan, baada ya kumuuwa ami wa baba yake  alietambulika kwa jina la Badar bin Seif mwaka 1804, na kutawala baada ya kifo cha Seyyid Sultan.

Mwaka 1832, Seyyid Said alifanya maamuzi ya kuhamisha makao makuu ya ‘milki’ yake kutoka Mascat Oman kuja Zanzibar na kuufanya Mji Mkongwe kuwa ndiyo Mji Mkuu wa Milki ya Usultan wa Omani.

HAJI NASSOR, PEMBA