KIJANA aliyemlawiti mtoto wa kiume wa miaka 10 huko Ndagaa kichakani wilaya ya Kati Unguja, amehukumiwa kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka 10 na mahakama ya mkoa Mwera.

Adhabu hiyo imetolewa na Hakimu Khamis Ali Simai, mara baada ya kumtia hatiani mshitakiwa huyo, licha ya kuiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa mujibu wa kosa lake.

Mshitakiwa huyo ni Mtayo Mauga Ngosha (25) mkaazi wa Ndagaa, ambae alishitakiwa mahakamani hapo kwa kosa la kulawiti kinyume na kifungu cha 115 (1) cha sheria nambari 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.

Matayo alitenda kosa hilo Aprili 19 majira ya saa 3:00 za asubuhi huko Ndagaa Kichakani wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja, ambapo bila ya halali alimuingilia kinyume na maumbile mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 10, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Kabla ya mahakama kumpa adhabu hiyo, mshitakiwa aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa sababu ameshawahi kuugua kifua.

Kwa upande wa Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Ayoub Nassor, ameiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa kwa mujibu wa sheria.

Pia alisema kuugua kwake kifua sio sababu ya mahakama kushindwa kumpa adhabu, kwa sababu wakati anatekeleza unyama huo hakuwa akisumbuliwa na kitu chochote.

Hivyo mahakama imemhukumu kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka 10, huku ikitoa haki ya rufaa mahakama ya juu ikiwa kama kuna upande wowote ambao haukuridhika na hukumu pamoja na adhabu hiyo.