Msanii wa muziki, Alikiba alikuwa kimya kwa muda mrefu toka atangazwe na klabu ya Coastal Union ya Tanga kwamba ni mchezaji wao na atacheza ligi kuu ya Tanzania Bara msimu ujao.

Kwenye mitandao ya kijamii kumekuwa ni gumzo kila mmoja akijiuliza muimbaji huyo atawezaje kujigawa kwenye mpira na muziki kwa kuwa mpira unahitaji muda mwingi zaidi kukaa kambini.

Siku ya jana ilikuwa ni siku ya ndoa ya dada yake Alikiba, Zabibu Kiba ambapo MC wa sherehe hiyo MC Pilipili alimuuliza muimbaji huyo kuhusiana na kusajiliwa kwake katika klabu hiyo yenye makazi yake mkoani Tanga.

“Tutaongea Tanga,” alisema Alikiba.

Watu wake wa karibu wamedai kwamba kwa sasa muimbaji huyo hawezi kuzungumza chochote mpaka atakapofika kwenye timu yake hiyo na kuanza mazoezi.

Uongozi wa klabu hiyo ulitangaza kwamba umemsajili mchezaji huyo kwaajili ya kuimarisha safu yao ya ushambuliaji.