Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Issa Maige amemhukumu raia wa Kenya, Don Bosco Gichana, kifungo cha miaka mitano jela na kulipa faini ya Sh milioni 300 baada ya kukiri makosa mawili yaliyokuwa yakimkabili ya kutakatisha fedha haramu baada ya kusomewa upya mashitaka.

Gichana akiwa na washitakiwa wenzake watatu akiwemo wakili maarufu jijini Arusha, Medium Mwale wiki iliyopita alikiri kutenda makosa hayo aliposomewa upya mashitaka yake mbele ya Jaji Maige. Katika kosa la kwanza, Gichana alidaiwa kula njama na katika shitaka la pili, alidaiwa kutakatisha fedha haramu dola za Marekani milioni 5,296 ,327.25 hatua iliyofanya washitakiwa wenzake kumwona msaliti na kumpa kipigo kabla ya kuokolewa na askari Magereza na Polisi walipofikishwa mahakamani Alhamis.

Katika hukumu iliyosomwa saa 4 : 09 asubuhi na Jaji Maige, mshitakiwa huyo aliyekuwa akikabiliwa na mashitaka mawili ya kula njama na utakatishaji fedha alikutwa na hatia katika makosa yote mawili. Jaji Maige alimhukumu kwenda jela miaka mitano kwa shitaka la kwanza la kula njama na hukumu yake kwa kosa hilo inaanza kutumika siku alipokamatwa mwaka 2012 hatua iliyomfanya aachiwe awe huru.

Katika shitaka la pili la utakatishaji fedha haramu na uhujumu uchumi, Jaji alimkuta na hatia na alimpiga faini ya Sh milioni 300 katika hukumu hiyo iliyochukua nusu saa faini inayopaswa kulipwa ndani ya mwezi mmoja na akishindwa ndani ya muda huo, anapaswa kutumikia kifungo cha miaka mitano jela. Jaji Maige aliwauliza mawakili wa serikali kama wako tayari kuendelea na kesi jana kwa washitakiwa wengine watatu ambapo mawakili hao wakiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Oswald Tibabyakyomya, Hashimu Ngole na Materius Marandu walisema walikuwa tayari kuendelea na kesi hiyo.

Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Omary Omary walimwomba Jaji Maige kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 21, mwaka huu wajipange na wateja wao baada ya mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo kukiri. Jaji Maige alimuuliza wakili Mwandamizi wa Serikali Osward Tibabyakyomya kama ana pingamizi na wakili huyo wa serikali alidai mahakamani hapo kuwa hana pingamizi na Jaji Maige akakubaliana na ombi hilo na kesi kuahirishwa hadi Septemba 21, mwaka huu asubuhi kesi itakapoendelea kusikilizwa.

Kesi hiyo sasa imebakiwa na washitakiwa watatu, Mwale anayekabiliwa na mashitaka 46 ya utakatishaji fedha haramu, kugushi, kula njama, kujipatia mali iliyopatikana kwa udanganyifu makosa anayodaiwa kufanya nyakati tofauti kati ya mwaka 2009 na 2012 wakati wakijua wazi kufanya hivyo ni kosa la jinai. Mshitakiwa wa tatu, Boniface Mwimbwa ana mashitaka 11 ya kutakatisha fedha haramu na kula njama na wa nne Elias Ndejembi ana makosa sita yakiwemo ya kudaiwa kutakatishaji fedha haramu na kula njama.

Chanzo Habari leo.