Maafisa wanyamapori wamethibitisha kutokea kwa tukio la Bwana mmoja nchini Marekani kumuua Simba wa milimani ambaye alimshambulia ghafla mbugani ingawa mwanamme huyo amepata majeraha makubwa usoni na kwenye kiganja cha mkono.

Simba huyo dume alimvamia kwa nyuma bwana huyo ambaye hakutajwa jina lake katika Hifadhi ya Wanyama ya Colorado.

Bwana huyo alikuwa akifanya mazoezi kwenye ukanda maalum kwenye mbuga hiyo ambao hupendelewa kutumiwa na wakimbiaji wakati tukio hilo lilipomkuta.

Maafisa wanasema aligeuka nyuma baada ya kusikia mnurumo nyuma yake nap apo hapo simba huyo akamrukia usoni.

“Simba alimrukia mkimbiaji huyo, na kumng’ata usoni na kiganjani. Lakini alifanikiwa kujinasua kutoka kwenye makucha yake na kisha kumuua,” taarifa rasmi ya hifadhi hiyo imeeleza.

Baada ya kumuua Simba huyo, bwana huyo alifanikiwa kuondoka eneo la tukio mwenyewe na kwenda kuomba msaada.

“Majeraha aliyopata usoni, mikononi, miguuni na mgongoni ni makubwa lakini si ya kutishia uhai wake,” taarifa hiyo imeongeza.

Meneja wa hifadhi hiyo, Mark Leslie amesema kuwa katika tukio hilo mkimbiaji alitumia uwezo wake wote kujilinda dhidi ya Simba aliyemvamia.

“Alitumia ubavu wake wote kujiokoa. Ikitokea umevamiwa na Simba yakupasa utumie nguvu na maarifa yako yote kama bwwana huyu kujiokoa,” amesema.