Dereva teksi Mousa Twaleb amefikishwa mahakamani nchini Tanzania akihusishwa na tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini humo Mohammed Dewji ‘Mo’.

Twaleb amepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo Jumanne Mei 28, 2019 akikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kumteka Mo.

Mo alitekwa na watu wasiojulikana alfajiri ya Oktoba 11, 2018 wakati akielekea mazoezini katika Hoteli ya Colosseum iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Bilionea huyo aliachiliwa huru Oktoba 20 baada ya watu waliomteka kudaiwa kumtelekeza kwenye viwanja vya Gymkhana.

Makosa mengine mawili aliyoshtakiwa nayo Bw Twalib ni kutakatisha fedha na kujihusisha na genge la uhalifu

Polisi waliwakamata watu kadhaa kuhusiana na tukio hilo na kuwaachilia baada ya kupatikana kwa bilionea huyo.

Kwa mujibu wa maelezo ya polisi, watekaji wake walikuwa ni raia wa Afrika Kusini na awali walilenga kupata fedha japo ‘walimwachia kwa woga baada ya msako kushamiri.’

Polisi kwa mara ya kwanza walimuonesha kwa wanahabari bw Twalib Novemba 11, 2018 ikiwa ni mwezi mmoja toka kutekwa kwa Mo.

Mkuu wa polisi wa Dar es Salaam, kamanda Lazaro Mambosasa aliwaambia waandishi kuwa bwana huyo ambaye pia ni dalali ndiye aliyewakaribisha mjini watekaji wa Mo na kuwapangisha nyumba ambayo alidai kuwa waliitumia kumficha Mo baada ya kumteka.

“Huyu bwana ameshiriki mwanzo mwisho. Amewakodisha hapa (kwenye nyumba alipokuwa ametekwa Mo) na ndiye aliyetumika kuwachukua kutoka eneo walipomuacha Mo Dewji na aliwapeleka hadi (kituo cha mabasi Ubungo kwenda nje ya Dar es Salaam,” alisema Mambosasa.

Mwenendo wa upelelezi wa polisi juu ya tukio la kutekwa na kuachiliwa kwa Dewji umeibua maswali mengi nchini Tanzania.

Mwezi Machi mwaka huu, Rais wa Tanzania aliikosoa polisi hadharani kwa namna waliyoendesha upelelezi wao.

“Mtu aliyetekwa alikutwa Gymkhana usiku lakini watu wanajiuliza Mmhh aliendaje pale, lakini alipowekwa pale na bunduki zikaachwa pale, unajiuliza huyu mtekaji aliamua kuziacha je angekutana na polisi wanaotafuta njiani?” alihoji Magufuli.

“Baada ya siku chache tukaambiwa nyumba ya alimokuwa ametekwa ni hii hapa na aliyekuwa anawabeba wale watekaji ni huyu hapa, Watanzania tukawa tunasubiri kwamba huyu sasa ndio atakuwa kielelezo cha kupelekwa mahakamani tusikie kitakachotokea lakini kimya mpaka leo miezi imepita… Haya hata kama Watanzania watanyamaza lakini mioyo yao haitakuwa clear (safi).

CHANZO. BBC SWAHILI