Askari anayejiita Faru John ameripoti Kituo Kikuu cha Polisi cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kufuatia agizo la kamnda wa kanda hiyo kumtaka awasili hapo ambapo alikohojiwa kuhusiana na tuhuma za rushwa na kuruhusiwa kuondoka akaendelee na kazi.
Agizo hilo lilitolewa Jumapili na Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa kwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Peter Sima jumatatu hii awe amempeleka askari  hiyo anayejiita Faru John ambaye anatuhumiwa na wananchi wa Mbagala kwamba amekuwa akidai rushwa.
Kamanda Mambosasa pia ametoa wiki moja kwa Kaimu Kamanda Sima awe amefuatilia tuhuma za rushwa zilizowasilishwa kwake na wananchi.
Amesema askari huyo ataendelea kufuatiliwa ili kubaini ukweli wa tuhuma zilizotolewa dhidi yake na endapo zitathibitishwa taarifa zitawasilishwa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro na atachukuliwa hatua za kisheria.
“Kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Temeke alimleta huyu askari ambaye nimemuhoji na kumruhusu kuendelea na kazi wakati akiendelea kuchunguzwa ndani ya wiki moja,” amesema Kamanda Mambosasa.
Akizungumza na wakazi wa Mbagala, walilalamika wakidai askari huyo anayejiita Faru John amekuwa akiwakamata wafanyabiashara na kudai kwa nguvu rushwa ya Sh20,000.
Wananchi hao wamelalamika kuwa, mfanyabiashara ambaye hatoi fedha hizo hufungwa pingu na kuzungushwa usiku kucha akiwa kwenye gari la polisi.
Kamanda Mambosasa aliyekuwa akisikiliza kero za wananchi wa Mbagala Zakhem alisema Jeshi la Polisi haliwezi kuwa na askari anayejipa jina la mzaha, huku akiwakandamiza wananchi.