Anusurika kufa baada ya kujitumbukiza kisimani Kusini Unguja

Mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Maryam Hassan Ndundu mwenye umri wa miaka 48 amenusurika kufa baada ya kujitumbukiza Kisimani huko shehia ya Kiongoni Kijiji cha Makunduchi Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja.

Wakielezea jinsi tukio hilo lilivyotokea baadhi ya mashuhuda wamesema kuwa mtu huyo ambae ni mgonjwa wa akili alijitia katika kisima hicho mnamo majira ya saa 9 Alaasiri ambapo alikua akitokea nyumbani kwao anapoishi kijiji cha Rohombaya shehia ya Kiongoni.

Wananchi wa eneo hilo walifanikiwa kumuokoa na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Cottage Makunduchi kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Akiwa katika eneo la tukio Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amewashukuru wananchi wa eneo hilo kwa mashirikiano makubwa waliyoyaonesha katika kuokoa uhai wa Mama huyo na kuwataka wananchi kuwa na tahadhari kwakua nao karibu watu wenye matatizo ya akili ili kuwaepusha na madhara kama haya.

Hata hivyo amesema Serikali wilayani humo itachukua hatua ya kukifunika kisima hicho kwa vile hakitumiki ili kuepusha maafa.

Na: Rauhiya Mussa.