Mwakilishi wa Paje aiomba Serikali kuwachukulia hatua viongozi wanaotoa vibali vya ujenzi kinyume na sheria

Mwakilishi wa Jimbo la Paje Jaku Hashim Ayoub ameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya Viongozi wa Serikali wanaowapa amri wahusika kutoa vibali vya ujenzi kinyume na Sheria  ili kupunguza tatizo la migogoro ya ardhi inayoendelea katika jamii.

Akiuliza swali katika Mkutano wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Mwakilishi huyo amesema kuna baadhi ya viongozi wanachangia kwa kiasi kikubwa  kuongezeka kwa migogoro ya ardhi na kusababisha wananchi kukosa haki zao katika kumiliki ardhi kisheria.

Amesema wakati umefika kwa Serikali kufuatilia kwa makini ili kuwababini Viongozi  wanaokiuka sheria na maadili katika kazi zao ikiwemo kuvamia Ardhi na kuwapa amri wahusika kutoa vibali kinyume na utaratibu uliopo.

Akitoa ufafanuzi  juu ya suala hilo Naibu Waziri wa Ardhi ,Nyumba,Maji na Nishati Juma Makungu Juma amesema Serikali  haitamvumilia mtu yeyote wakiwemo viongozi ambao watabainika kujihusisha na migogoro ya ardhi ili kuwawezesha wananchi kunufaika na rasilimali ya Ardhi kisheria.

Amesema katika kukabiliana na tatizo hilo serikali imeunda kamati maalumu ya udhibiti wa Ujenzi  (DCU) ili kufuatilia matumizi mabaya ya Rasilimali Ardhi yanayofanywa katika jamii.

Naibu Makungu ametoa wito kwa Wananchi kuacha kununua Ardhi kinyume na Sheria ili kujiepusha na matatizo yasiyo ya lazima ikiwemo kuuziwa ardhi katika njia za maji ya mvua pamoja na kuzuiwa kujenga na Serikali.

Na;Fat-hiya Shehe Zanzibar24.

fathiyashehe@gmail.com