Usiku wa Jana ulikuwa Mgumu kwa Mbwana Samatta na Timu yake ya Aston Villa walipokaribishwa na Wenyeji wao Leicester City katika dimba la King Power na hatimaye wakajikuta wakichakazwa kwa kipigo cha goli 4-0.

Kipigo kinazidi kuiporomosha Aston Villa inayofundishwa na kocha Muingereza, Dean Smith sasa ikibaki na pointi zake 25 baada ya kucheza mechi 28 na kuendelea kukamata nafas ya 19, ikiizidi pointi nne Norwich City inayoshika mkia katika ligi ambayo mwisho wa msimu timu tatu zitateremka daraja. 

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Michael Oliver, mabao ya Leicester City inayofundishwa na kocha wa zamani wa Liverpool, Brendan Rodgers yalifungwa na Harvey Barnes dakika ya 40 na 85 na Jamie Vardy mawili pia, dakika ya 63 kwa penalti na 79.


Kwa ushindi huo, Leicester City inafikisha pointi 53 baada ya kucheza mechi 29 na kuendelea kukamata nafasi ya tatu, nyuma ya Manchester City yenye pointi 57 za mechi 28 na Liverpool yenye pointi 82 za mechi 29.