Maumbile ya watu wenye kimo kifupi kisicho cha kawaida maarufu kama mbilikimo au vibete yanatufanya kuitwe ‘watoto’ kila wanapopita ilhali ni watu wazima.

Hali ya kimo kifupi inafafanuliwa na kikundi cha utetezi wa watu wafupi nchini Marekani kama urefu wa watu wazima wenye futi nne nchi 10 au chini yake, kutokana na matibabu au maumbile.

Ingawa vikundi vingine vinaweza kupanua vigezo vya aina fulani za ufupi hadi futi 5. h

Wastani wa mtu mzima mwenye hali hiyo ni futi nne.

Bi Mueni ambaye jina lake la utani ni (Princess Confidence) ana miaka 29, na alizaliwa na kimo hicho ambapo mbele ya jamii yeye huonekana kuwa ni msichana mdogo au hata mtu mwenye ulemavu fulani.

Hata hivyo hayuko pekee, Julie Waithera Karanja ana miaka 30, yeye pia ni mbilikimo, hali inayomfanya kukabiliana na changamoto chungu nzima katika maisha ya kawaida .

Wanawake hawa wawili wanatoka jijini Nairobi Kenya na hii ni taarifa inayowahusu.

Ruth Mweni
Mueni ni miongoni mwa watu wafupi kupitia kiasi ambao wamekubali hali yao licha ya changamoto wanazokumbana nazo

Bila shaka kimo chao kinafanya maisha yao kuwa ya aina yake , kwa kuwa wanawake wenzao walio na kimo cha kawaida wana mambo wanayoweza kuyafanya lakini ambayo kwao ni changamoto.

Lakini hilo haliwavunji moyo kamwe kwani wameyapokea maumbile yao kama sehemu inayowafanya kuwavutia wengine kutokana na umbo lao la kipekee .

Bi Mueni alieleza: “Wakati wa usafi wa kawaida nyumbani utapata kuwa maeneo yalio juu mimi siwezi kuyafikia , na lazima nitumie ngazi au kiti ” kwa mfano ninapotaka kusugua kuta za nyumba.

Bi Mueni hatahivyo anasema kwamba changamoto hizo ni za kawaida sana matamshi yanayoungwa mkono na mwenzake Bi Julie.

Julie anasema kwamba wakati wanapotafuta usafiri wa umma , wao hubebwa juu ili kuingia ndani ya magari kwa kuwa hawawezi kufikia ngazi za kuingia katika magari hayo.

“Wakati tunapoingia katika magari ya umma ambayo nchini Kenya yanajulikana kama matatu , utapata kuna baadhi ya wahudumu wa magari wanatuinua juu-juu kana kwamba sisi ni watoto wadogo huku abiria wengine wakijitolea kutupakata iwapo magari hayo yamejaa”

Ruth Mueni anaelezea kwamba changamoto kuu ya hali yao huwapata wakati wanapotafuta wapenzi. Anasema kwamba wanawake wenye vimo vifupi hubaguliwa zaidi kuliko wenzao wa kiume.

Anasema kuwa sio rahisi kwa baadhi yao kupata wapenzi kutokana na kejeli na utani unaozunguka suala zima la kuchumbiwa.

“Baadhi ya wanaume hawataki kuonekana wakitembea na mwanamke mfupi kama mimi, unampata mwanamume anavutiwa nami lakini anafanya mzaha kuhusu maumbile yangu!

Anasema kwamba kutokana na uzoefu alionao anaona jamii inawatizama kama wanawake ambao hawajakamilika kimaumbile , na hapo ndipo maswali mengi huibuka. iwapo wanawake wenye kimo kifupi kuliko kawaida wana uwezo wa kujifungua watoto au hata kuwa na uwezo wa kuhimili kukuza familia? na kadhalika .

Bi , Diana Waithera amejaaliwa mtoto mmoja , lakini ijapokuwa hakutaka kuzungumzia mazingira ya hali yake ya kimapenzi anakubali kuwa wanawake wenye kimo kifupi wanabaguliwa sana na wanaume.

Anasema kwamba ni wanawake wachache wenye hali kama yake waliopo katika ndoa licha ya kwamba pia nao wana hisia kama wanawake wengine wowote.

“Sio jambo rahisi kupata mwanamke mwenye kimo kifupi kwenye ndoa ni wachache mno hali hii imechangiwa na jinsi tunatizamwa kwenye jamii , sisi pia tunazo hisia kama wanawake wengine na inakera sana mtu anapokufananisha na mtoto na hilo lina kuwa kiini kikubwa cha kwanini sisi tunaona vigumu kuwa na mchumba “Diana alisema.

Huku dunia ikiadhimisha siku ya walemavu duniani, watu wenye kimo kifupi kupitia kiasi pia wametambulika katika makundi ya walemavu kwani kimo chao kifupi kinakuwa kikwazo kikuu katika mambo mengi ya maisha ya kawaida.

Licha ya hayo, kikundi hiki cha watu kinataka kitambuliwe na kina jizatiti sana kama Bi Mueni aliyeteuliwa kuwania tuzo la malkia wa urembo la Miss Confidence tawi la Kenya.

Mbali na hayo mwanamke huyo pia amebobea katika mchezo wa Parabadminton ambapo aliishindia Kenya nishani ya dhahabu baada ya kuiwakilisha.

Vilevile Ruth Mueni ndiye mwanzilishi wa chama cha watu wanaoishi na kimo kifupi nchini Kenya .

Bila shaka wote wanakubaliana kuwa kabla hawajajikubali walivyo kimaumbile , walikuwa wanapitia vipindi vigumu hapo awali kwa kukosa kujiamini na kujikubali.

Kikubwa wanachosema ni kuwa watu wanaoishi na ulemavu wowote hususan wanawake wanapaswa kukubali hali zao kwa haraka kwani kimsingi ni kuwa mwanamke wa kawaida anayepigania nafasi yake ili kutambuliwa katika jamii.

Kila siku wanatafuta njia za kujiimarisha kimaisha kwa kutumia vipaji vyao au kazi za mikono yao ili kufanikisha maisha yao bila kutegemea mtu yeyote.