Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) Dk. Mohamed Seif Khatib amesema mashirikiyano baina ya Baraza hilo na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) yamefanikiwa kukuza lugha ya Kiswahili .

Hayo ameyasema huko katika Ofisi ya BAKIZA  Mwanakwerekwe  wakati alipokuwa akizungumza na watendaji wa Mabaraza yote mawili kuhusu mafanikio yaliyopatikana  kwa kufanya kazi kwa ushirikiano

Amesema Mabaraza hayo yamekuwa yakifanya kazi kwa pamoja katika kukuza lugha ya Kiswahili ambapo hivi sasa  lugha ya Kiswahili imepiga hatua kubwa na kuzungumzwa katika mataifa mbali mbali Duniani.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar Dk. Mwanahija Ali Juma  amesema lengo la  vikao vya pamoja ambavyo hufanyika kila mwaka vina lengo la kujadiliana na kuendeleza ushirikiano katika kukikuza Kiswahili.

Aliongeza kuwa vikao hivyo vimfanikiwa kwa kiasi kikubwa kuendeleza istilahi, ufasaha na usahihi katika matumizi ya Kiswahili kwa watu wa ndani na nje ya nchi kujifunza lugha kwa urahisi hiyo.

“Mashirikiyano haya yameweza kutuweka pamoja na kutatua changamoto zinazojitokeza  kwenye matumizi ya lugha ya  Kiswahili na lugha hiyo kusonga mbele,” alisema Dk. Mwanahija Ali Juma.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili la Tanzani Consalata Mushi amesema kuwepo kwa mashirikiyano ya pamoja yameweza kuleta tija kubwa katika  kuendeleza matumizi ya lugha ya Kiswahili.

Amesema lugha ya Kiswahili imepiga hatua kwa kuongeza misamiati kuzidisha fursa kwa waandishi wa habari na kutumika kwa ufasaha kwa watunzi wa vitabu nchini.

Aliongeza kuwa hivi sasa imeleta fursa ya Watanzania wengi kwenda  kwenda kufundisha katika vyuo mbali mbali vilioko nje ya Nchi.

Amesema vikao hivyo ambavyo vimekuwa vya kawaida kfanyika kila mwaka vinatoa fursa ya kujadiliana juu ya kukuza lugha ya Kiswahili na changamoto zinazojitokeza na kuzipatia ufumbuzi kupitia mabaraza hayo mawili. 

Mwashungi Tahir  –  Maelezo Zanzibar.