Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema ushirikiano wa pamoja wa Wagunbe wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wa Majimbo yaliyomo ndani ya Mkoa wa Shinyanga chini ya usimamizi wa Serikali umesaidia kupaisha kwa kasi kubwa Mkoa huo Kimaendeleo ndani ya kipindi kifupi.

Balozi Seif Ali Iddi amesema hayo wakati akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Kishapu akimalizia ziara yake ya Siku Tatu Mkoani Shinyanga akiwa Mlezi wa Mkoa huo kuangalia umaliziaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015-2020 ndani ya Mkoa huo.

Amesema Waheshimiwa Wabunge wa Majimbo hayo wakiwa Watumishi wa Wananchi walionyesha ukomavu mkubwa uliopelekea  kuhamasishana katika kuona changamoto zinazowakabili Wananchi katika Majimbo yao zinapata ufumbuzi wa kudumu.

Hata hivyo Balozi Seif akiwa pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Hamashauri Kuu ya Taifa ya CCM ameonyesha kuchukizwa kwake na tabia ya baadhi ya Wabunge wa Majimbo kuwachukia wenzao wa Viti Maalum wa Mikoa pale wanaposhiriki katika kuunga mkono Wananchi kwenye Miradi yao ya Maendeleo.

alisisitiza kwamba itapendeza na kufurahisha pale Mbunge wa Viti Maalum ambae yeye ni Mtumishi wa Wananchi wa Majimbo ya Mkoa mzina napoamua kupeleka maendeleo ni vizuri kumuarifu Mbunge Muhusika wa Jimbo ili kazi zao ziwe na maingikliano ya pamoja.

Akizungumzia muelekeo wa Taifa katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Mwezi Oktoba Mwaka huu Balozi Seif aliwakumbusha Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuelewa kwamba wao ndio waamuzi wa kumchagua Kiongozi atakayepaswa kuwaongoza ndani ya Miaka Mitano ijayo.

Akigusia Uchaguzi wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Seif alisema Dr. John Pombe Magufuli ameshaonyesha wazi moyo wake wa kukubali kuendelea kuwatumikia Watanzania Bara na Zanzibar katika kipindi chengine kijacho.

Aliwaagiza Viongozi wa ngazi zote ndani ya Mkoa wa Shinyanga kusimamia ipasavyo kampeni za kistaarabu zitakazomuwezesha Dr. Magufuli kwenye uchguzi ujao kuibuka kwa asilimia 100% ya kura zote ikilinganishwa na asilimia 68% ya Kura alizozipata kwenye uchaguzi wa Mwaka 2015.

Wakielezea Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 – 2020 Wabunge wa  Majimbo yaliyomo ndani ya Mkoa wa Shinyanga pamoja na wale wa Viti Maalum wamempongeza na kumshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kwa kasi kubwa anayoisimamia katika kuimarisha Uchumi wa Taifa.