Balozi Seif aagiza kuondolewa Makontena katika eneo la bandari Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi wa Shirika la Bandari Zanzibar kuyaondosha mara moja Makontena yote yaliyopo katika maeneo ya Bandari ambayo hayana bidhaa ili kuondoa vurumai liliyopo katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdullah Juma Abdullah alisema Bandari hiyo hupokea Makontena elfu 5,000 yanayoingia kila Mwezi ambapo uwezo wa Bandari ni Makontena elfu 4,180.

Balozi Seif amesema hatua hiyo mbali ya kuondoa msongamano katika eneo hilo muhimu lakini pia itasaidia kuchukuwa hadhari mapema kabla ya kusubiri kutokea athari inayoweza kusababishwa na uzito wa Makontena yanayoteremshwa katika Bandari hiyo.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa Agizo hilo wakati alipofanya ziara ya ghafla Bandarini Malindi mapema Jana kuangalia mazingira halisi ya utendaji kazi pamoja na kuona mrundikano wa Makontena ambayo kama haikuchukuliwa hatua za dharura yanaweza kuleta athari hapo baadae.

Alisema katika jitihada za kuwaona Watendaji wa Shirika hilo wanawajibika ipasavyo ni vyema kwa Uongozi wa Shirika kuchukuwa hatua za kuwatoza kodi za ziada wafanyakazi wote watakaochelewa kutoa Makontena yao Bandarini kwa mujibu wa Taratibu zilizowekwa.

Balozi Seif  aliushauri Uongozi wa Shirika hilo kulitumia eneo la pembezoni mwa Hoteli ya Bwawani ambalo kipindi cha nyuma walikuwa wakilitumia kuweka Makontena kwa vile ujenzi wa eneo hilo katika masuala ya Uwekezaji bado haujakamilika Kisheria.

Alisema mrundikano wa idadi kubwa ya Makontena kupindukia uwezo wa eneo hilo unaweza kuleta athari kubwa ya kudidimia au kukatika kwa Bandari hiyo iliyojengwa kwa gharama kubwa mno na Serikali Kuu.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdullah Juma Abdullah alisema Bandari hiyo hupokea Makontena elfu 5,000 yanayoingia kila Mwezi ambapo uwezo wa Bandari ni Makontena elfu 4,180.

Alisema hivi sasa yapo Makontena 2,302 Bandarini kati ya hayo 185 matupu yakiwemo yale ya ziada 400 yanayopaswa kuhamishwa ndani ya eneo hilo la Bandari.

Mkurugenzi Abdullah alimueleza Balozi Seif  kwamba wapo baadhi ya Wafanyabiashara waliokuwa na tabia ya kuifanya bandari kama sehemu ya kuweka Makontena yao lakini mpango huo hivi sasa umetafutiwa dawa kwa mujibu wa utaratibu wa Bandari.

Alisema watendaji wa Shirika hilo kupitia Mkuu wa Operesheni wanajiandaa kuitumia fursa ya kuyahifadhi Makontena matupu katika eneo liliopo mbele ya Hoteli ya Bwawani ili kutekeleza agizo hilo.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.