Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa wito kwa Watu wote  wanaomiliki Vyombo vya usafiri vya Majini na Barabarani  kuzingatia sheria na kanuni zote za usalama wa abiria ili kunusuru maisha ya Wananchi na mali zao pale wanapotumia vyombo hivyo.

Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiahirisha Mkutano wa Kumi na Moja wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa ukifanyika katika Ukumbi wa Majengo ya Baraza hilo uliopo Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif Ali Iddi alisema uzoefu unaonyesha kwamba ajali nyingi zinazoripotiwa kutokea hapa Nchini zinatokana na uzembe pamoja na ukiukwaji wa makusudi wa Sheria za usalama wa vyombo husika.

Alisema Serikali katika kuendelea kuzingatia wajibu wake itaendelea kusimamia ipasavyo sheria hizo  za usalama wa vyombo vya usafiri Majini na Nchi kavu bila ya kumuonea muhali Mtu ye yote atakayekwenda kinyume na sheria zilizopo.

Balozi Seif alieleza kwamba Utulivu na Amani ya moyo miongoni mwa Wananchi inaweza kutetereka endapo Sheria na Taratibu za Nchi hazitazingatiwa na kukiukwa kama inavyoonekana hofu iliyotanda kwa kundi la Wanawake na Watoto lililovamiwa kwa kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.

Alisema Jamii inayowadhalilisha na kuwanyanyasa Wanawake na Watoto kamwe haiwezi kupata maendeleo ya haraka kwa vile hukosa thamani na heshima mbele ya macho ya Jamii nyengine iwe ndani au nje ya Nchi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya Akina Baba wa kisasa wanaoamua kuacha jukumu lao la Malezi na badala yake kujiingiza katika kundi la wadhalilishaji  Watoto wao wa kuwazaa pamoja na wale wanaowalea.

Alisema vitendo hivyo ni vya Kinyama na vya kiaibu kwa Jamii yenye kufuata Mila, Desturi, Silka na Utamaduni. Hivyo aliwataka Wazee wenye hulka kama hiyo wabadilike ili kuwapa faraja Watoto wao wanaopaswa kupata furaha na amani katika maisha yao ya kila siku.

Balozi Seif alitanabahisha kwamba Ulezi wa zamani wa kuwaacha Watoto pekee Majumbani hivi sasa umepitwa mno na wakati kwa vile unatoa fursa kwa wahalifu kuitumia nafasi kama hiyo kutekeleza vitendo vyao viovu vya udhalilishaji.

Akizungumzia migogoro ya Ardhi iliyopo Nchini katika maeneo mengi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali itaendelea kuifuatilia kwa karibu zaidi migogoro hiyo ili kutafuta mbinu na namna ya kuitatua.

Alisema hatua zimeanza kuchukuliwa katika kuziimarisha Mahkama za Ardhi, kuwaelimisha Viongozi wa ngazi tofauti wakiwemo Masheha na Wananchi ili kuondosha au kupunguza kwa kiasi kikubwa kadhia hiyo.

Balozi Seif alifahamisha kwamba ni jambo la kusikitisha kwa uwepo wa ushahidi wa vielelezo unaoonyesha kwamba bado wapo baadhi ya Watendaji wa Umma wasio waaminifu katika Taasisi zinazosimamia Ardhi wanaokiuka taratibu za Kiutumishi.

Alisema Watumishi hao hudiriki kutoa nyaraka zaidi ya Moja kwa Kiwanja Kimoja jambo linalosababisha kuwa kiini cha migogoro baina ya Wananchi tatizo linalokwenda sambamba na ucheleweshwaji wa makusudi wa hati za Viwanja kwa Wananchi.

Kuhusu Dawa za Kulevya  ambazo ni janga linaloendelea kuikumba Dunia Hivi sasa Balozi Seif Ali Iddi aliwanasihi Wananchi kuachana na kujishirikisha katika Uingizaji, usambazaji, Uuzaji na utumiaji wa Dawa hizo thakili kwa Maisha yao.

Alieleza kwamba Dawa za Kulevya tayari zimeshaleta  athari kubwa inayolikumba zaidi kundi kubwa la Vijana ambalo ndio nguvu kazi kubwa ya inayotegemewa na Taifa wakati wowote ule.

Balozi Seif alizikumbusha Taasisi zote Nchini hasa zaidi zile zinazohusika na udhibiti wa mapambano dhidi ya uingizaji na usambazaji wa Dawa hizo kuendelea  kuimarisha mashirikiano yao katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwa kutokomeza janga hilo.

“ Viongozi kwa kushirikiana na Wananchi na Wadau wote tuendelee kushikamana katika mapambano dhidi ya janga hili kwani Zanzibar bila ya Dawa za kulevya inawezekana kabisa kama tutatia nia thabiti”. Alisisitiza Balozi Seif.

Alisema Serikali kwa upande wake itaongeza jitihada za mapambano yake dhidi ya wale wanaojihusisha na tatizo hilo na kamwe haitamuonea muhali Mtu au Kiongozi ye yote atakayeshindwa kutimiza wajibu wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewashukuru Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kutumia nafasi yao ya Kidemokrasia ya kuisimamia, kuishauri na kuihoji Serikali jambo ambalo limeonyesha  nia thabiti waliyonayo ya kuitaka Serikali kuwajibika ipasavyo kwa Wananchi wake.

Balozi Seif aliwaomba Wajumbe hao wa Baraza la Wawakilishi waendelee kupendana, kuvumiliana na kushirikiana katika kulijenga Taifa Kiuchumi na Kijamii, kwani mshikamano na Umoja huo ndio utakaolivusha Taifa hili kuelekea kwenye Maendeleo makini.

Aliema pamoja na Maswali ya Msingi 154 yaliyoulizwa na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kujibiwa na Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri Mkutano huo pia Wajumbe hao walipata fursa ya kujadili Miswada Mitatu na baadae kupitishwa kuwa sheria.

Aliitaja Miswada hiyo kuwa ni pamoja na Mswada wa Sheria ya Kuweka Masharti Bora ya Usimamizi wa Mahkama, kufafanua Utumishi wa Mahkama, Kuanzisha Ofisi za Mtendaji Mkuu wa Mahkama na MraJIS, Kuanzisha Mfuko wa Mahkama na kuweka Masharti mengine yanayohusiana na hayo.

Mengine ni Mswada wa Sheria ya kuanzisha Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Elimu na kuweka Masharti ya Mkaguzi wa Elimu pamoja na Mambo mengine yanayohusiana na hayo  na ule Mswada wa Sheria wa Kuanzisha Wakala wa Serikali wa Uchapaji Zanzibar na kuweka Masharti Bora yanayohusiana na Kazi, Uwezo, Uongozi na Mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Alsema Miswada hiyo Mitatu iliyojadiliwa na kupitishwa kwa Kauli moja itasaidia kuimarisha Utawala Boa ikiwemo Uwajibikaji kwa Watendaji wa Taasisi za Umma kwa lengo la kukuza Uchumi wa Taifa.

Balozi Seif aliwaomba Wananchi wote kutoa ushirikiano wa karibu wakati Miswada hiyo itakapoanza kuwa Sheria na kutambua wazi kwamba Sheria wakati wote hutungwa kwa ajili ya kusimamia Haki za Wananchi wake na kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

“ Tutambue kuwa Sheria Siku zote zinatungwa kwa ajili ya kusimamia Haki za Wananchi wake kwa Maendeleo yao na Taifa lao kwa ujumla”. Alisisitiza Balozi Seif.

Baraza la Wawakilishi Zanzibar liemahirishwa hadi Jumatano ya Tarehe 28 Novemba Mwaka 2018.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.