Waziri wa Kilimo wa Cuba Bwana Guastavo Rodriguez Roller akipokea zawadi ya Mlango wa Zanzibar kutoka kwa Balozi Seif  kama ishara ya kufunguliwa Mlango wa ukaribu zaidi na Zanzibar katika ushirikiano wa Wizara yake na ile ya Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Serikali ya Cuba kupitia Wizara yake inayosimamia Sekta ya Kilimo na Mifugo kwa mtazamo wake wa  kuanzisha ushirikiano mpana zaidi na Zanzibar na Tanzania katika Sekta hiyo muhimu.

Alisema kitendo cha Cuba kutoa fursa ya upendeleo kwa kuualika Ujumbe wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kushiriki katika Maonyesho ya Kimataifa ya Kilimo Mjini Havana kimeonyesha mwanzo wa ufunguzi wa ukurasa mwengine wa ushirikiano katika sekta tofauti.

Akizungumza na Waziri wa Kilimo wa Jamuhuri ya Cuba Bwana Guastavo Rodriguez Roller Makao Makuu ya Wizara hiyo Mjini Havana, Balozi Seif  alisema Zanzibar na Cuba zimekuwa na mafungamano ya karibu katika Sekta za Afya na Elimu kwa kipindi kirefu sasa yaliyoleta mafanikio makubwa.

Balozi Seif alisema kwa vile Maonyesho ni moja ya njia ya kubadilishana mawazo Kitaaluma alimuomba na kumualika Waziri wa Kilimo wa Cuba kutenge muda wa kushiriki Maonyesho ya Kimataifa ya Tanzania yanayofanyika  Mwezi wa Agosti wa Kila Mwaka Nchini Tanzania.

“ Ushiriki wa Maonyuesho mbali mbali popote pale hutoa fursa kwa wadau kujifunza mambo tofauti yanayosaidia kutoa muelekeo bora wa Ushirikiano”. Alisema Balozi Seif.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha uhusiano wa Kihistoria uliojengeka baina ya Mataifa hayo Marafiki kwa zaidi ya Miaka Hamsini sasa kupitia Waasisi wake Marehemu Baba wa Taifa Mwalim Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Marehemu Fidel Castro wa Cuba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza umuhimu wa kuanzisha ushirikiano mpya wa kilimo cha Miwa katika muelekeo wa kuendeleza Sekta ya Viwanda kwa vile Cuba na Tanzania zinafanana kwa hali ya hewa zake.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dr. Makame Ali Ussi alisema upo umuhimu wa kutiliwa mkazo suala la Uwekezaji katika Sekta ya Viwanda sambamba na Taaluma ya kuyalinda Mazao ya mizizi yanayoonekana kukumbwa na maradhi tofauti.

Dr. Makame alisema umuhimu huo utaongeza uhusiano wa kirafiki uliyopo baina ya Zanzibar na Cuba kufuatia utiaji Saini Mkataba wa Ushirikiano wa pande hizo mbili karibu Miaka Mitano iliyopita katika Sekta za Afya na Elimu.

Alisema Wizara ya Kilimo, Malisili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar kupitia Idara na Taasisi zake inaendelea kuimarisha kilimo cha Mpunga na mazo mengine ya biashara, Mifugo, Malisili na uvuvi ili kutanua wigo wa ajira sambamba na kuongeza mapato ya Taifa na Mwananchi Mmoja Mmoja.

Aidha Naibu Waziri wa Kilimo huyo wa Zanzibar alisema mkazo utaongezwa katika kuimarisha Kitengo cha Utafiti kitakachokuwa na uwezo na nguvu zaidi za kutoa taarifa za muelekeo wa Kitaalamu katika Sekta hiyo.

Mapema Waziri wa Kilimo wa Jamuhuri ya Cuba Bwana Guastavo Rodriguez Roller Cuba imebarikiwa kuwa na Hekta Milioni 10,000,000 zilizopelekea kutoa ajira kwa Wakulima zaidi ya Elfu 5,000.

Alisema asilimia 70% ya Ardhi hiyo imechukuliwa na Maliasili, asilimia 3.5% Mifugo ambapo zaidi ya asilimia 60% inakwenda uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na Kilimo pekee.

Bwana Guastavo alisema Serikali ya Cuba katika mpango wake wa muda mrefu imejikita kuimarisha zaidi Viwanda vya Sukari, ukulima wa Mpunga pamoja na Kunde vyakula vinavyopendwa na Wananchi walo wengi Nchini humo.

Alieleza kuwa Sera ya Taifa la Jamuhuri ya  Cuba ni kuimarisha Ustawi wa Watoto wake kwa kuwapatia lishe bora ya maziwa na nyama walio chini ya Miaka Saba.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

19/03/2019.