Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema miradi ya Kijamii inayoendeshwa kupitia Mfuko wa wa Maendeleo ya Jamii Tanaznia  {TASAF }  inalazimika kukabiliwa na wananchi wenyewe katika maeneo yao kwa vile wao ndio wanaoelewa mazingira yanayowazunguuka.

Alisema Serikali Kuu kazi yake kubwa ni kuongeza nguvu za uwezeshaji katika kuona miradi hiyo inaimarika na kukua kwa lengo la kuwaondoshea ukali wa maisha Wananchi wake katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya
Unguja na Pemba.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo akiwa katika ziara ya siku Tatuni Kisiwani Pemba kuangalia miradi ya Maendeleo wakati alipokagua miradi ya Tasaf katika Bonde la Kidau Ndagoni kuona maendeleo ya ujenzi wa Tuta la kuzuia maji ya Bahari yanayoathiri wakulima wa bonde hilo.

Alisema yapo maendeleo makubwa yaliyopatikana tokea kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) hasa katika kuzisaidia Kaya Maskini zilizozongwa na ukali wa maisha ziwe na miundombinu ya kujiendesha Kimaisha kupitia miradi wanayoianzisha.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wananchi na wakulima hao wa Bonde la Kidau pamoja na wale wote wanaopata huduma kupitia mfuko wa Tasaf  kutokana na juhudi kubwa wanazozichukuwa katika kuimarisha miradi yao ikiwemo ile ya sekta ya kilimo iliyokuwa tegemeo kubwa la wananchi wa Zanzibar kwa zaidi ya asilimia  8%.

Akitoa ufafanuzi wa kitaalamu wa ujenzi wa Tuta hilo la kuzuia maji ya bahari katika Bonde la Kidau  Ndagoni Mhandisi wa Wizra ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi nd. Talib Bakari alisema zaidi ya Eka 33 kwenye Bonde hilo zimekuwa zikiingia Maji ya Bahari.

Nd. Bakari alisema hali hiyo imewafanya Wakulima wapatao  92 wameathirika na tatizo hilo lililopelekea kukosa kuendelea na harakati zao za kilimo cha Munga pamoja na mazao mengine ya nafaka.

Mhandisi Bakari alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba athari hiyo iliyokuwa kero kwa wakulima hao na pia kuchangia uharibifu wa mazingira ilipeklekea wananchi na Wakulima hao kuwamua ujenzi wa
Tuta ili kunusuru hali hiyo.

Alisema ujenzi wa Tuta hilo la kuzuia maji ya Bahari ambao kwa sasa umeshafikia asilimia 90% unaotarajiwa kuchukuwa siku 45 hadi kukamilika kwake utaweza kuwafaidisha Wakulima 92.

Alifafanua kwamba gharama za ujenzi wa Tuta hilo utafikia jumla ya shilingi Milioni 37,000,000/- ambazo kati ya hizo Milioni 30,000,000/- zimewagusa Wananchi wenyewe wa Kaya Maskini na zilizobakia milioni 7
zimepangwa kuhudumia wafanyakazi ambao wengine ni miongoni mwao.

Mapema Mkulima Maisuri Omar Suleiman kwa niaba ya wakulima wenzake wa Bonde hilo la Kidau Ndagoni wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake wa kuwapatia mradi wa Tasaf ambao wameueleza kuwa umeleta ukombozi mkubwa kwao.

Mkulima Maisuri alisema wakulima na wananchi wa Vijiji vilivyo jitrani na Bonde hilo wamepata faraja kubwa kupitia Mfuko wa Tasaf  jambo ambalo kwa kiasi kuikubwa wamefanikiwa kupunguza ukali wa maisha na kujiongezea kipato kinachoashiria kusaidia familia zao.

Hata hivyo Mkulima Maisuni kwa niaba ya wakulima na wananchi wenzake wameiomba Serikali Kuu kufikiria kuwaongezea uwezeshaji zaidi kwa ajili ya kuendesha miradi mengine ya maendeleo na kiuchumi ili kufikia
malengo yao waliyojipangia.