Balozi Seif awapa onyo watendaji wa Hospitali ya Abdullah Mzee Pemba

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameonya kuwa atamuwajibisha Kiongozi au Mtendaji yeyote wa Wizara ya Afya atakayehusika na ucheleweshaji wa ununuzi wa Vifaa vya kupoza Umeme kwa ajili ya Mashine za Maabara ya Hospitali ya Abdullah Mzee Mkoani.

Balozi Seif akipata maelezo kutoka kwa Mmoja wa Watendaji wa Vitengo vya uchunguzi wa Afya katika Hospitali ya Rifaa ya Mkoani kuona mashine iliyosita kufanya kazi kutokana na sababu za ukosefu wa vifaa vya kupozea Umeme.

Balozi Seif alitoa onyo hilo alipofika kuangalia uwajibikaji wa Watendaji katika kutoa Huduma za Afya kwa Wananchi katika Hospitali ya Rufaa ya Abdullah Mzee Mkoani ikiwa ni utaratibu wake aliojipangia wa mara kwa mara anapofanya ziara Kisiwani Pemba huitembelea hospital hiyo.

Amesema inasikitisha kuona Serikali Kuu kwa kusaidiana na Washirika wa Maendeleo inajitahidi kuimarisha Miundombinu katika Sekta ya Afya kwa lengo la kutoa huduma sahihi za Afya lakini wapo baadhi ya watumishi wamekuwa na tabia ya kuleta dharau katika matumizi ya Vifaa wanavyopatiwa.

“ Nikija tena katika ziara zangu za mara kwa mara kama havijawekwa Vifaa vya  kupoza Umeme unaoingia katika Mashine za Maabara nitalazimika kuchukuwa hatua zinazostahiki kwa Mtendaji mzembe”. Alisisitiza Balozi Seif.

Alisema Serikali katika jitihada zake za kuimarisha Sekta ya Afya kwa kugharamia  ununuzi wa vifaa vya kisasa  vyenye thamani kubwa isingependa kuona zipo dalili zinazoashiria hujuma za makusudi zinazojaribu kukwamisha jitihada hizo muhimu kwa ustawi wa Jamii.

Mapema Mkuu wa Kitengo cha Maabara katika Hospitali hiyo Dr. Mohamed Mjaka Khamis alisema changamoto kubwa inayowakumba katika utendaji wao wa kila siku ni kuzimika kwa Umeme mara kwa mara hali inayosababisha baadhi ya Mashine za Maabara hiyo kuharibika kutokana na ukosefu wa Vifaa vya kupoza Umeme kwa ajili ya ulinzi wa Mashine za Maabara ya Hospitali hiyo.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi alikagua Maendeleo hya Ujenzi wa Jengo Jipya la Skuli ya Sekondari ya Uweleni iliyopo ndani ya Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba unaofanywa kwa Nguvu za Wananchi wanaoungwa Mkono na Washirika mbali mbali wa Maendeleo ndani na nje ya Nchi.

Akizungumza na Uongozi wa Skuli hiyo Balozi Seif  alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutafuta wafadhili ili kuona changamoto inayowakwaza Wanafunzi wa Skuli hiyo ya uhaba wa Madasrasa inatanzuka.

Alisema Sera ya Elimu Zanzibar katika Miundombinu ya ujenzi wa Majengo ya Madarsa sehemu mbali mbali Unguja na Pemba ni kwa Wizara husika ya Elimu na Mafunzo ya Amali kukamilisha uwezekaji pamoja na samani za ndani kwa Madarasa yote yaliyoanzishwa na Wananchi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wananchi, Wazai,Walimu, pamoja na wafadhili wa Wilaya ya Mkoanuikutokana na hamasa zao za muamko uliopelekea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuimarisha Sekta ya Elimu Nchini.

Balozi Seif alisisitiza kwamba hakuna mtaji  au Rasilmali kubwa na muhimu ambayo mzazi anaweza kuwekeza kwa Mtoto wake isipokuwa Elimu ambayo ndio njia sahihi ya kumjengea hatma njema wakati wa Uzee wake.

Mapema akitoa Taarifa ya ujenzi wa Jengo Jipya la Skuli ya Sekondari ya Uweleni Mwalimu Mkuu wa Skuli Hiyo Shehe Hassan alisema wazo lka ujenzi huo limekuja kufuatia changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili Wanmafunzi wa Skuli hiyo ya ufinyu wa Madarasa.

Mwalimu Shehe alisema Uongozi wa Skuli hiyo kwa kushirikiana na Wazazi wa Wanafunzi hao walilazimika kuanza michango iliyotokana na Mishahara yao kuanza ujeni huo ili ukidhi mahitaji ya ongezeko la Wanafunzi waliofikia Elifu 1,149 hivi sasa wanaolazimika kuingia Mikondo Miwili.

Alisema ujenzi  wa jengo hilo utakaokuwa na Madarasa Sita, Ukumbi wa Mikutano pamoja na Ofisi ya Walimu ulianza mnamo Mwaka 2011, lakini changamoto liliopo hivi sasa ni umaliziaji wa tofali za juu pamoja na ukuta wa kuhifadhia Jengo hilo.

Akitoa shukrani zake Waziri wa Elimu na Mfunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma aliuahidi Uongozi wa Skuli hiyo pamoja na Wazazi wa Uweleni kwamba Wizara ya Elimu itabeba jukumu la kumaliza kazi iliyobakia.

Alisema licha ya jukumu la Wizara kumalizia uwezekaji na samani ya Vifaa vya ndani lakini imekubali kusidia nguvu kutokana na jitihada kubwa iliyotekelezwa na Wazazi, Viongozi na Walimu katika kujenga Jengo hilo jipya la Skuli ya Uweleni ili kupunguza msongamano wa Wanafunzi wake.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

12/10/2018.