Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewatahadharisha Wananchi kuzingatia kwamba Karantini wanaowekewa Watu walioingia Nchini kutoka Nje ya Nchi sio adhabu  bali ni utaratibu unaozingatia Muongozo wa Wataalamu wa Afya katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona vinavyosababisha Mafua na Homa Kali ya Mapafu.

Alisema yeye akiwa Kiongozi wa Serikali alilazimika kutii muongozo huo kufuatia ziara yake Maalum aliyoifanya Nchini Cuba hivi karibuni ambapo wakati anarejea Nchini Muongozo huo tayari unafanya kazi.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa tahadhari hiyo leo huko Nyumbani Kwake Mtaa wa Kama Kaskazini Kidogo ya Mji wa Zanzibar  wakati akitoa Taarifa kwa Umma baada ya kumaliza muda wake wa wa mapumziko Siku 14 zinazomuwajibika Kila Msafiri aliyeingia Nchini kutoka nje ya Nchi kwa mujibu wa Wataalamu.

Hata hivyo Balozi Seif alisema kwa mujibu wa Wataalamu wa Sekta ya Afya walimshauri aendelee kuongeza Siku Saba Zaidi ili kumaliza vyema Karantini hiyo.

Amewakumbusha Wananchi kuacha utamaduni wa mazoea Kwa kuepuka Mikusanyiko isiyo ya laizima na pale inapobidi ni vyema wazingatia muongozo wa Afya kwa kuvaa vifaa maluum vya kuziba Midomona pua sambamba na kunawa mikono kila wakati kwa kutumia maji ya kutiririka.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Mawaziri wa Afya wa Serikali ya Muungano waTanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada wanazoendelea kuzichukuwa katika kuipatia Jamii Taarifa sahihi juu ya muenendo mzima wa Virusi vya Corona.