Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Jamii bado inapaswa kuchukuwa tahadhari ya kuendelea kujikinga na maambukizi ya Virusi hatari vya Corona  vilivyoleta fadhaa ndani ya Jamii Kitaifa sambamba na Jumuiya ya Kimataifa.

Amesema Corona ilileta hofu, wasi wasi na simanzi Dunia nzima  hali iliyopelekea baadhi ya Mila na Taratibu za Wanaadamu kama vile kupeana mikono kuachwa kwa muda ili kuepuka maambukizi ya janga hilo thakili.

Balozi Seif Ali Iddi akiwa pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda anayemaliza Muda wake alisema hayo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi Vifaa vya kinga dhidi ya Virusi vya Corona  kwa matumizi ya Walimu na Wanafunzi wa Skuli  12 zilizomo ndani ya Jimbo hilo hafla iliyofanyika katika Skuli ya Sekondari Kitope.     

Alieleza kwamba Jamii kuendelea kujikinga na Maambukizi ya Virusi vya Corona bado itakuwa ni suala la lazima katika kipindi hichi cha mpito kwa vile maradhi yanayotokana na Virusi hivyo yanaendelea kuitesa Dunia katika baadhi ya Mataifa zikiwemo Nchi za Bara la Afrika.

Hata hivyo Serikali ililazimika kupunguza masharti Kumi yaliyoainishwa kupunguza Maambukizi ya Vurusi hivyo baada ya jihitada kubwa iliyochukuliwa na Taifa kwa kushirikiana na Wananchi pamoja na Taasisi za Kitaifa na zile za Kimataifa.

“ Hatua za kunawa Mikono kwa maji ya kutiririka, vitakasa Mikono na uvaaji wa Maski katika maeneo ya msongamano ni vyema ikaendelea kuzingatiwa na kufanywa kama suala la kawaida katika Jamii”. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru na kuwapongeza Wananchi wote Nchini kwa usikivu wao uliopelekea kufuata maelekezo ya Serikali Kuu pamoja na Wataalamu wa Sekta ya Afya na hatimae Taifa kuendelea kubakia salama.

“ Tuna mfano wa Majirani wenzetu wa Mataifa ya Madagaska na Botswana waliofanikiwa kudhibiti kuendea kwa maambukizi ya Virusi vya Corona na kuamua kulegea vikwazo kwa hatua kubwa ambayo sasa inawagharimu kutokana na kasi kubwa ya kurejea upya kwa Maambukizi ya Virusi hivyo”. Alitanabahisha Balozi Seif.

Alisisitiza umuhimu wa Wanafunzi na Walimu Maskulini kuendelea kuvitumia Vifaa vya Kinga kutokana na maeneo yao makubwa kuendelea kuwa na msongamano mkubwa wa Watu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Wananchi hao kwa vile yeye anapumzika Utumishi wa Jimbo washirikiane na Viongozi wao wa Mahonda Mpya iliyokuja baada ya marekebisho ya Mipaka iliyofanywa hivi karibuni na Tume ya Uchaguzi Zanzibar {ZEC}.

Mapema Katibu Tawala wa Wilaya ya Kaskazini “B” Nd.  Makame Machano Haji kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo Nd. Rajab Ali Rajab alimshukuru Balozi Seif kwa kukamilisha ahadi alizotoa wakati wa Utumishi wake unaomalizika hivi karibuni.