Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi amesema wakati umefika kwa Wanawake Nchini kujitokeza kuwania nafasi mbali mbali za Uongozi ndani ya Majimbo yao ili kujiwekea nguvu zaidi za kuelekea kwenye asilimia 50% katika maeneo ya maamuzi.

Amesema tabia ya Wanawake waliowengi Nchini kukimbilia kwenye nafasi za Viti Maalum endapo hawataachana nayo inaweza kuwalete usumbufu kwa kusingizia mfumo Dume sambamba na kuviza ile kiu yao ya kufikia malengo ya Hamsini kwa Hamsini na Wanaume.

Akizungumza na Wajumbe wa Halmashauriu Kuu ya CCM ya Mkoa wa Kusini Pemba kwenye Ukumbi wa Makonyo Wawi Chake chake Pemba Balozi Seif alisema wapo baadhi ya Wanawake wamejihalalishia zile nafasi za Viti Maalum kitendo ambacho kinawanyima fursa Wanawake wenzao hasa wale Vijana.

Balozi Seif amesema Taifa kupitia Sekta ya Elimu tayari imeshazalisha wanawake wengi wenye uwezo wa Kitaaluma na nguvu za kuwatumikia Wananchi lakini wengi kati yao wanashindwa kujitokeza kwa kuhofia nguvu kubwa waliyonayo Wanaume pamoja na udhaifu wa Kijinsia Majimboni

“  wanawake lazima wathubutu kuingia katika mchakato wa Majimbo badala ya kulemaa katika Viti Maalum na hii huchangia kuondoa wale wenye tabia ya kununa pale wanaposhindwa katika uchaguzi”. Alisema Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

Balozi Seif amewapongeza wale wanasiasa wa Vyama vyengine vya upinzani walioamua wenyewe kujiunga  na wengine kurejea Chama cha Mapinduzi kilichoonyesha msimamo wake wa kusimamia Ilani ya Uchaguzi ambayo hivi sasa kila Mwananchi amekuwa shahidi wa Maendeleo hayo.

Aliwahakikishia wale wote waliojiunga na Chama cha Mapinduzi kutokana na Sera zake inazotekelezeka watapewa ushirikiano mkubwa utakaosaidia kuongeza nguvu za CCM katika kuwatumikia Wananchi waliowengi bila ya kujali tofauti za Kidini na Kisiasa.

Amesema ni vyema Jamii ikaelewa kwamba Ofisi yake ambayo kwa sasa imekuwa ikipokea malalamiko mengi ya Vijana wanaohitaji Ajira haina fursa hiyo kwa vile utaratibu wa ajira unasimamiwa na Taasisi inayohusika na masuala ya Utumishi wa Umma Serikalini.

Katika Kikao nhicho Mjumbe huyo wa Kamati Kuu Balozi Seif alimpokea aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Chake Chake kupitia Chama cha Wananchi {CUF} Mh. Kaiza Yussuf  ambae aliamua rasmi kujiunga na Chama cha Mapinduzi .

Akitoa salamu mara baada ya kukabidhiwa Kadi ya CCM pamoja na kula kiapo aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Chake Chake kupitia Chama cha Wananchi {CUF} Kaiza Yussuf Makame alisema amefikia uamuzi wa kujiunga na Chama cha Mapinduzi kutokana na Ilani yake kutekelezeka na kuwagusa Wananchi wa aina zote Nchini.

Mh. Kaiza amesema haamini kama kuna upinzani wa Kisiasa Nchini Tanzania katika kipindi cha Miaka 50 iliyopita na uamuzi wake wa kuacha upinzani umempa faraja kubwa itakayojenga Historia Mpya kwake kwa kukabidhiwa Kadi ya CCM ndani ya Kikao Kizito cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa.