BARAZA La Manispaa Mjini limewataka wafanyabishara katika eneo la viwanja vya sikukuu kuwa waaminifu na kuuza bidhaa zenye ubora ambazo hazitaathiri afya za mlaji.

Ofisa uhusiano wa baraza hilo, Hassan Yahya Hassan, aliyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake Malindi.

Alisema kuuza bidhaa zenye ubora na zenye viwango itasaidia kulinda afya ya mtumiaji.

Alisema maandalizi ya viwanja vyote vinavyotumiwa na wafanyabiashara  katika kipindi cha sikukuu tayari yamekamilika kwa asilimia 90, vikiwemo viwanja vya Mmazimmoja.

Hivyo aliwaomba wafanyabiashara kufuata maelekezo yote yaliyowekwa na baraza la manispaa wakati wanajisajili kupata vibali vya kufanyia biashara.

Aliwaaomba wananchi kushirikiana pamoja katika kuweka mji safi na endapo atabainika mtu anachafua mazingira kwa makusudi hatua za kisheria zitachuliwa dhidi yake.

“Niwaeleze kuwa harakati za sikukuu zikiwa zinaendelea pamoja na shughuli za uchumi ni vyema tukaitumia miundombinu ya usafi tuliyoiweka ili kudhibiti uchafuzi wa mji wetu,” alisema.

Aidha aliwasisitiza wazazi na walezi kuwa makini na watoto wanaofika katika viwanja vya sikukuu kwa kuwasimamia vizuri watoto wao.