Baraza la Mitihani la Tanzania limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha sita uliofanyika mwezi Mei mwaka huu ambapo kwa wastani skuli zote zilizofanya mtihani huo zimefanya vizuri.

Akitoa taarifa mbele ya waandishi wa habari katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mazizini, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania Charles Msonde alisema watahiniwa wa kike wamefanya vizuri zaidi ukilinganisha na wanaume .

Alisema watahiniwa wa shule waliofaulu ni 78,666 sawa na asilimia 99.14 na watahiniwa wa kujitegemea 9,403 wamefaulu ikiwa ni sawa na asilimia 91,95.

Alisema takwimu za ufaulu kwa watahiniwa wa shule umepanda kwa masomo mengi mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana isipokuwa masomo ya General Study, History, Biology na Accountancy.

Dkt.  Msonde aliongeza kuwa ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliopata watahiniwa wa shule unaonyesha kuwa jumla ya watahiniwa 76,655 sawa na asilimia 96.61 wamefaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu.

Alizitaja Shule 10 bora Kitaifa kuwa ni Kisimiri ya Arusha, Fedha Boys ya Dar es salaam, Ahmes ya Pwani, Mwandet ya Arusha, Tabora Boys ya Tabora, Kibaha ya Pwani, Fedha Girls ya Dar es salaam, ST, Marys Mazinde juu ya Tanga, Cannosa ya Dar es salaam na Kemebos ya Kagera.

Alimtaja mwanafunzi bora Kitaifa mwaka huu kwa masomo ya Sayansi ni Faith Nicholous Matee kutoka shule ya ST. Marys Mazinde juu ya Tanga.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani amewapongeza walimu na wanafunzi wote wa shule zilizofanya mtihani wa kidato cha sita kwa juhudi kubwa walizochukua  na kupata matokeo mazuri mwaka huu.