Siku moja baada ya kurejea hewani kwa wimbo wa Mwanza uliopigwa marufuku, Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), limetishia kumfungia mwanamuziki huyo iwapo litajiridhisha amekiuka maagizo aliyopewa.

Hata hivyo, uongozi wa mwanamuziki huyo umekiri kuliona hilo lakini umekanusha kuhusika na kurejeshwa kwake katika mtandao wa Youtube.

Wimbo wa Rayvanny kutoka lebo ya Wasafi alioimba na Diamond Platnumz, ulifungiwa Novemba 12 mwaka huu baada ya kubainika kuwa maneno yake yanaenda kinyume na maadili ya Kitanzania.

Rayvanny aliamriwa auondoe wimbo huo sambamba na kutozwa faini ya Sh9 milioni kwa kuutoa wimbo bila kufuata taratibu.

Jana video ya wimbo huo imeonekana kurudi katika mtandao huo wa Youtube.

Katibu wa Basata, Godfrey Mngereza, amesema hawajauruhusu wimbo huo kurudishwa na haitatokea uruhusiwe kwa kuwa haufai kuendelea kusikilizwa na jamii.

Amesema kama ni masuala ya kiufundi mwenye dhamana ya kuhakikisha hauonekani ni wasanii wenyewe na kuonya kuwa kama watashindwa watawachukulia hatua zaidi za kinidhamu ikiwemo kuwafungia wasijishughulishe na kazi za sanaa.

Kwa upande wake Meneja wa lebo ya Wasafi, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ amekiri kuiona video hiyo na kueleza kuwa si wao walioirudisha bali kuna mtu anafanya hivyo.

Amesema wameshatoa taarifa Basata kuhusu tatizo hilo na pia wana mpango wa kuomba msaada kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kitengo cha makosa ya kimtandao nchini ili waweze kuwasaidia kutatua jambo hilo.

“Sisi hatupo tayari kukwaruzana na Basata katika hilo, kama nilivyosema awali tutahakikisha tunatekeleza maagizo yao yote, hata yanayotokea ya video kurudi lipo nje ya uwezo wetu katika masuala ya kiufundi zaidi kwani kila tukiitoa kuna mtu anairudisha, tumeshaanza kuwasiliana na mamlaka za masuala ya mitandao kulishughulikia hilo,’ amesema Babu Tale.