tdb

Bodi ya maziwa  Tanzania (TDB) imeeleza kuwa maziwa ya unga ambayo yanatokana na viwandani si salama kiafya kutokana na namna ya utengenezaji na njia inayotumika hadi kumfikia mtumiaji.

Watendaji wakuu wa bodi hiyo ya maziwa wakizungumza na wanahabari mapema leo Jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa taarifa yao ya utendaji, Majukumu, mafanikio na changamoto, mikakati na mipango yao waliweza kufafanua mambo mbalimbali ikiwemo suala hilo la maziwa ya Unga ambayo si salama kwa afya licha ya kuwepo kwa wingi katika soko la ndani.

Akijibu swali la mwandishi wa mtandao huu kuhusiana na usalama wa maziwa ya unga ambayo yapo hapa nchini, Msajili wa maziwa wa bodi hiyo, Bw. Nelson Kilongozi alifafanua kuwa, Maziwa ya unga kimsingi yanatengenezwa kutoka maziwa yenyewe halisi viwandani na kuwa unga kisha kumfikia mlaji.

Hata hivyo tatizo ya maziwa hayo ya unga ni pale yanapochanganywa viwandani ili kumfikia mlaji kwani yanaongezwa vitu ama yanapunguzwa hivyo kwa wakati mwingine kusababisha matatizo na kuwa si salama kwa mtumiaji hii ni pamoja na kwa watoto wadogo ama mtu aliye mgonjwa.

“Maziwa yakiwa mengi na mafuta yanakuwa kidogo. Na maziwa yakiwa kidogo na mafuta yanakuwa mengi hivyo katika ubora ule wa awali unapungua. Unaweza kukuta low fat baada ya asilia moja unakuta asilimia tatu” alifafanua, Bw Kilongozi

Hata hivyo, Kilongozi aliongeza kuwa, Bodi inaweka sharia na masharti mengi ya kuzuia maziwa hayo ili kulinda soko la ndani la maziwa.

Suala linguine ambalo Bodi hilo iliweza kulifafanua ni maeneo yanayozalisha maziwa kwa wingi ni pamoja na maeneo mbalimbali ikiwemo maeneo makubwa manne ikiwemo Kaskazini-Manyara Arusha na Kilimanjaro. Pwani-Morogoro Tanga na Dar es Salaam. Nyanda za juukusini-Iringa, Mbeya, Songwe.

Pia kuna maeneo ya Kanda ya Ziwa- Kagera, Mwanza na Shinyanga, hata hivyo mikoa ya Nyanda za Juu kusini ndiyo inazalisha kwa wingi sana kwa asilimia 40 na kufuatia mikoa ya ukanda wa Kaskazini.

Bodi hiyo imeeleza kuwa,  Tasnia ya Maziwa ni moja ya tasnia muhimu katika sekta yaa mifugo na inachangia takribani theluthi moja ya mapato yanayotokana na sekta hiyo.

Hadi sasa Tanzania inakadiliwa kuwa na ng’ombe wapatao Milioni 25.8 na kati ya hao, takribani 720,000 ni ng’ombe wa kisasa (pure breed) au chotara wake. Hata hivyo Bodi hiyo inaeleza kuwa uzalishaji wa maziwa hapa nchini umekuwa ukiongezeka kila mwaka na unafikia lita Bilioni 2.06  kwa mwaka 2014/2015 na asilimia 70 ya maziwa hayo uzalishwa na ng’ombe wa asili ambao ufugwa katika mfumo wa asili na asilimia 30 iliyobaki uzalishwa kwa ng’ombe wa kisasa au Chotara.