Hakuna yeyote anayependa kuwa na ugonjwa ni kikwazo na ni chanzo cha gharama. Unapokuwa mgonjwa, huhisi tu vibaya bali pia huenda ukashindwa kwenda kazini au shuleni, kutafuta pesa, au kuitunza familia yako. Huenda hata ukahitaji mtu fulani akutunze, na huenda ukahitaji kulipia gharama za dawa na matibabu.

Kuna msemo usemao “Kinga ni bora kuliko tiba.” Baadhi ya magonjwa hayaepukiki. Hata hivyo, bado kuna mambo mengi unayoweza kufanya ili kupunguza au hata kuzuia kuanza kwa ugonjwa. Fikiria mambo matano unayoweza kufanya ili kuwa na afya bora.

Unapaswa kunawa mikono: Baada ya kutoka chooni, Baada ya kumbadilisha nepi mtoto au kumsaidia kutumia choo, Kabla na baada ya kutibu jeraha au kidonda, Kabla na baada ya kumtembelea mgonjwa, Kabla ya kutayarisha, kuhudumia, au kula chakula, Baada ya kupiga chafya, kukohoa, au kupenga kamasi, Baada ya kumgusa mnyama au kinyesi cha mnyama,Baada ya kutupa takataka.

Usifikiri kwamba kunawa mikono yako kikamili ni jambo lisilo muhimu. Uchunguzi umeonyesha kwamba asilimia kubwa ya wale wanaotumia vyoo vya umma hawanawi mikono yao vizuri au hawanawi kabisa.

Unapaswa kunawa mikono yako jinsi gani?

Rowesha mikono yako katika maji safi ya bomba na kisha utumie sabuni, Sugua mikono yako pamoja ili kupata povu, bila kusahau kusafisha kucha, vidole, pande zote za mkono, na katikati mwa vidole vyako, Endelea kusugua kwa sekunde 20 hivi, Safisha mikono yako katika maji safi yanayotiririka, Kausha mikono yako kwa kutumia kitambaa safi au karatasi ya kukaushia mikono.

Ni rahisi kufanya mambo hayo, na kufanya hivyo kunaweza kuzuia ugonjwa na kuokoa uhai.[

Mara nyingi mtu huambukizwa ugonjwa wa kipindupindu baada ya kunywa maji au kula chakula kilicho na viini kutoka kwa watu walioambukizwa.

Unaweza kuchukua hatua gani ili kujilinda hata baada ya kupatwa na ugonjwa au maambukizo mengine yanayotokana na maji yasiyo salama?

Hakikisha kwamba maji unayokunywa, kutia ndani maji unayotumia kusafisha meno, kugandisha barafu, kusafisha chakula na vyombo, au kupikia, yanatoka kwenye chanzo salama, kama vile bomba la umma, lenye maji yaliyowekwa dawa ili kuua viini au maji ya chupa yanayotengenezwa na kampuni inayoaminika.

Ikiwa maji ya bomba unayotumia si safi, chemsha maji kabla ya kutumia au weka dawa ya kuua viini.

Unapotumia kemikali au dawa za kuua viini katika maji, kama vile klorini au dawa za kusafisha maji, fuata maelekezo ya watengenezaji.

Tumia mashine ya kuchujia maji iliyo bora ikiwa inapatikana na ikiwa unaweza kununua.

Ikiwa hakuna dawa za kuua viini katika maji, tumia dawa ya kuondoa madoa, weka matone mawili katika lita moja ya maji, changanya vizuri, na kisha acha maji yatulie kwa dakika 30 kabla ya kuyatumia.

Sikuzote hifadhi maji safi katika vyombo vilivyo safi na ufunike ili kuzuia yasichafuliwe kwa njia yoyote.

Hakikisha kwamba vyombo vinavyotumiwa kuchota maji kama vile kikombe ni safi.

Mikono yako inapaswa kuwa safi unapotumia au unapogusa vyombo vinavyotumiwa kutunza maji, na usitumbukize mikono yako au vidole katika maji ya kunywa.

     KULA CHAKULA KINACHOFAA

Mtu anahitaji chakula chenye lishe bora ili awe na afya nzuri. Huenda ukahitaji kuchunguza matumizi yako ya chumvi, vyakula vyenye mafuta, sukari, na unapaswa kujua kiasi cha chakula unachokula. Unapokula tumia pia matunda, mboga, na uwe na kawaida ya kula vyakula vya aina mbalimbali. Soma maelezo yaliyo katika pakiti ya bidhaa ili uweze kununua vyakula vya nafaka ambayo haijakobolewa kama vile mkate, nafaka yenyewe, tambi, au mchele. Vyakula hivi vina virutubisho na nyuzinyuzi kuliko vyakula vinavyotokana na nafaka zilizokobolewa. Ili kupata protini, kula kiasi kidogo cha nyama ya ng’ombe na kuku, na ikiwezekana jitahidi kula samaki mara kadhaa kwa juma. Katika nchi fulani ni rahisi kupata vyakula vyenye protini kutoka kwenye mboga.

Ukiwa na zoea la kula vyakula vyenye sukari nyingi na mafuta yaliyoganda, unaweza kunenepa kupita kiasi. Ili kuepuka hilo, kunywa maji badala ya vinywaji vyenye sukari. Kula matunda zaidi badala ya vyakula vyenye sukari. Punguza kiasi cha vyakula vyenye mafuta unachotumia kama vile soseji, nyama, siagi, keki, jibini, na biskuti. Na badala ya kupika kwa kutumia mafuta yaliyoganda, lingekuwa jambo linalofaa kutumia mafuta yanayofaa mwili.

Kutumia chumvi au sodiamu kupita kiasi unapokula, kunaweza kuongeza shinikizo la damu kwa kiwango kisichofaa kwa mwili. Ikiwa una tatizo hilo, soma maelezo yaliyo katika pakiti ya chakula ili ujue jinsi ya kudhibiti matumizi yako ya sodiamu. Badala ya kutumia chumvi, tumia vikolezo na viungo ili kufanya chakula chako kiwe na ladha.

Kiasi unachokula kina umuhimu sawa na chakula unachokula. Hivyo, usiendelee kula chakula ikiwa tayari umeshiba, hata kama unafurahia kula chakula hicho.

Jambo lingine kuhusu lishe ni hatari ya kula chakula kisichofaa. Chakula chochote kisipotayarishwa na kutunzwa vizuri kinaweza kukuletea madhara. Kila mwaka, mtu 1 kati ya 6 nchini Marekani anaugua kutokana na kula chakula kisichofaa. Wengi wao hupona kwa muda mfupi, hata hivyo kuna wachache wanaokufa.

Unaweza kufanya nini ili kuepuka hatari hiyo?

Kwa kuwa mboga hukuzwa katika udongo ambao huenda umewekwa mbolea, safisha vizuri mboga kabla ya kupika.

Safisha kwa maji moto yenye sabuni, mikono yako, ubao unaotumia kukatia mboga, vyombo, na kaunta za jikoni kabla ya kuanza kuandaa chakula.

Ili kuepuka kuchafua chakula safi, epuka kukiweka katika sahani au chombo chochote kisichosafishwa kilichokuwa kimetumiwa kuweka mayai mabichi, kuku, nyama, au samaki.

Pika chakula vizuri na tunza mara moja katika friji vyakula vyovyote vinavyoweza kuharibika ikiwa unapanga kula baadaye.

Tupa chakula chochote kinachoweza kuharibika kilichoachwa kwa zaidi ya saa mbili au moja katika hali ya hewa inayozidi nyuzi joto 32.

      FANYA MAZOEZI

BILA kujali umri wako, unahitaji kufanya mazoezi kwa ukawaida ili uwe na afya nzuri. Watu wengi leo hawafanyi mazoezi ya kutosha. Kwa nini ni muhimu kufanya mazoezi? Kwa sababu kufanya mazoezi kunaweza kukusaidia:

 • Kulala vizuri.
 • Kuweza kutembea kwa wepesi.
 • Kuwa na mifupa na misuli yenye nguvu.
 • Kudumisha au kuwa na uzito wa mwili unaofaa kiafya.
 • Kupunguza hatari ya kuwa na ugonjwa wa kushuka moyo.
 • Kupunguza hatari ya kufa mapema.

Ikiwa haufanyi mazoezi, huenda ukapatwa na:

 • Ugonjwa wa moyo.
 • Ugonjwa wa kisukari aina ya 2.
 • Kupatwa na shinikizo la damu.
 • Mwili kuwa na kiwango cha juu cha kolesteroli.
 • Kupatwa na kiharusi.

Kwa kuwa mazoezi yanayofaa yanategemea umri na afya ya mtu, ni vizuri kuwasiliana na daktari wako kabla ya kuanza kufanya mazoezi yoyote mapya. Kulingana na mapendekezo mbalimbali, watoto na vijana wanapaswa kutumia angalau dakika 60 kila siku kufanya mazoezi rahisi na magumu. Watu wazima wanapaswa kutumia dakika 150 za mazoezi rahisi au dakika 75 za mazoezi magumu kila juma.

Fanya mazoezi utakayofurahia. Unaweza kucheza mpira wa kikapu, tenisi, mpira wa miguu, kutembea haraka, kuendesha baiskeli, kulima bustani, kukata kuni, kuogelea, kupiga kasia mtumbwi, kukimbia polepole, au mazoezi yoyote ya viungo. Utajuaje kwamba mazoezi ni rahisi au ni magumu? Kwa ujumla mazoezi rahisi hukufanya utoe jasho, lakini magumu ni yale ambayo unapoyafanya inakuwa vigumu kwako kuzungumza.

      LALA VYA KUTOSHA

Kiasi kinachohitajika cha usingizi kinatofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine. Watoto wengi wachanga hulala saa 16 hadi 18 kwa siku, watoto kuanzia umri wa mwaka mmoja hadi mitatu hulala saa 14 na wale wenye umri wa miaka mitatu hadi minne hulala saa 11 au 12 hivi. Watoto walio na umri wa kutosha kwenda shule kwa ujumla wanahitaji kulala kwa saa 10, vijana kwa saa 9 au 10, na watu wazima kwa saa 7 hadi 8.

Kulala vya kutosha hakupaswi kuonwa kuwa ni uamuzi tu wa mtu. Kulingana na wataalamu, kulala vya kutosha ni muhimu kwa ajili ya:

 • Ukuzi na maendeleo ya watoto na vijana.
 • Kujifunza na kukumbuka habari mpya.
 • Kudumisha usawaziko unaofaa wa homoni zinazosaidia kumeng’enya chakula na uzito wa mwili.
 • Kudumisha moyo wenye afya nzuri.
 • Kuzuia magonjwa.

Kutolala vya kutosha kumetajwa kuwa chanzo cha kunenepa kupita kiasi, kushuka moyo, ugonjwa wa moyo, kisukari na chanzo cha aksidenti mbaya. Bila shaka, mambo hayo yanatufanya tuwe na sababu nzuri za kuhakikisha kwamba tunalala vya kutosha.

Hivyo, ufanye nini ukigundua kwamba haulali vya kutosha?

 • Lala na amka muda uleule kila siku.
 • Jitahidi kufanya chumba chako cha kulala kiwe na utulivu, chenye giza, cha kustarehesha, na kisiwe na joto au baridi sana.
 • Usitazame Televisheni au kutumia kifaa cha kielektroniki unapokuwa kitandani.
 • Jitahidi kadiri uwezavyo kufanya kitanda chako kiwe chenye kustarehesha.
 • Epuka kula vyakula vizito, kafeini, na kileo kabla ya kulala.
 • Ikiwa hata baada ya kufuata mapendekezo hayo bado unakosa usingizi au una magonjwa mengine yanayohusiana na usingizi kama vile kulala au kusinzia kupita kiasi mchana au kupumua kwa shida unapolala, huenda ikafaa zaidi kumwona daktari.