HATUA ya Jamhuri ya Brazil kufungua ubalozi mdogo visiwani Zanzibar, mbali na kuimarisha uhusiano wa nchi mbili hizo, pia itaongeza fursa za uwekezaji na ushirikiano  wa kiuchumi na biashara.

Wakwanza kushoto aliyekaa ni Balozi mdogo wa Brazil hapa zanzibar ni Abdulsamad Abdulrahman Wapili aliyesimama ni Waziri wa nchi ofisi ya rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi Gavu alitoa shukrani kwa niaba ya SMZ kutipia msaada uliotolewa na Serikali ya Brazil na wa tatu alikaa ni Balozi mkubwa wa Tanzania Carlos Alfonso.

Akizungumza juzi katika hafla ya ufunguzi wa ubalozi huo uliopo Kikwajuni mjini Zanzibar, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Barza la Mapinduzi Issa Haji Gavu, amesema sasa milango kwa wawekezaji kutoka Brazil itazidi kufunguka.

Alieleza pamoja na hatua hiyo kuimarisha uhusiano kati ya nchi mbili hizi, lakini pia wawekezaji wa Brazil na Zanzibar watapata uwanja mpana wa kuangalia maeneo zaidi wanayoweza kushirikiana katika kukuza uchumi wa nchi zao.

Waziri huyo alifahamisha kuwa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilikuwa na hamu kubwa kuona Brazil inafanya kazi nayo kwa karibu, ili iweze kufaidika na utaalamu wa watu wake katika nyanja mbalimbali za kiuchuni, kiutamaduni, kimichezo na nyengine  kadhaa.

“Brazil ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, michezo hasa mpira wa miguu, uchimbaji na uendelezaji nishati za gesi na mafuta, hivyo tunatarajia kuwepo ubalizi wao hapa, kutainufaisha nchi yetu na utaalamu wao,” alifafanua.

Aidha, alisema uamuzi huo umepokelewa kwa mikono miwili kwa kuwa hiyo ni hamu na shauku aliyokuwa nayo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa muda mrefu.

Aliahidi kuwa serikali itatoa kila aina ya ushirikiano kwa Balozi wa heshima na watendaji walio chini yake, kuhakikisha wanatekeleza vyema majukumu yao na kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar na Brazil kwa manufaa ya sasa na baadae.

Mapema, Balozi wa Brazil nchini Tanzania Carlos Alfonso, alisema kufungua ofisi za ubalozi mdogo hapa Zanzibar, ni miongoni mwa mambo ambayo Rais Dk. Shein aliiomba nchi yake wakati alipokutana naye mwezi Machi 2017, Ikulu mjini Zanzibar.

Aliyataja mambo mengine ambayo Zanzibar imetaka kushirikiana kwa karibu  na Brazilk ni katika sekta ya biashara na afya.

“Nina furaha kusema kwamba, tayari tumefanikisha ufunguzi wa ubalozi mdogo, pia tumeweza kuleta wawekezaji kutoka Brazil wanaoendelea kufanya kazi hapa, pamoja na kuleta timu ya wataalamu wa sekta ya afya katika mradi wa afya ya uzazi na mtoto,” alieleza Balozi Alfonso.

Alisema tayari wataalamu hao wametembelea hospitali ya Mnazimmoja, Kivunge na Kidongo Chekundu, pamoja na kufanya mazungumzo na Waziri wa Afya wa Zanzibar Hamad Rashid Mohammed, juu ya namna bora ya kusaidia uimarishaji huduma za afya hapa nchini.

Aidha alisema, nchi yake imefadhili safari na ushiriki wa Daktari mmoja kutoka hospitali ya Mnazimmoja, kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa dunia utakaowakutanisha madaktari bingwa wa maradhi ya wanawake, unaotarajiwa kufanyika jijini Rio De Janeiro Oktoba 15 hadi 26, 2018.

Balozi Alfonso, alifahamisha kuwa nchi yake ina mpango wa kuanzisha ushirikiano katika sekta ya utalii, kwa kuvitangaza vivutio vilivyopo Zanzibar ili kuwashawishi Wabrazili kufika hapa, na pia Wazanzibari kuanzisha uhusiano wa kibiashara na wenzao wa huko.

Kwa upande wake, Balozi wa heshima atakayeiongoza ofisi hiyo ambaye ni Mzanzibari Abdulsamad Abdulrahim, pamoja na kuishukuru serikali ya Brazil kwa kumuamini na kumkabidhi wadhifa huyo, aliahidi kufanya kila jitihada kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya nchi mbili hizo.

Alisema kuna mambo mengi ambayo nchi hizo  zinaweza kushirikiana kwa manufaa ya wananchi wao, ikiwemo uwekezaji katika sekta ya utalii, biashara, mafuta na gesi asilia.

Aidha, alisema miongoni mwa vipaumbele vyake, n kuona jitihada zinafanyika kuhakikisha Zanzibar inanufaika na utaalamu wa sekta ya viwanda walionao Wabrazili, ili kwenda na kasi ya uchumi wa viwanda ambayo Tanzania ya sasa inakazania.

Balozi huyo pia alisema, atatumia utajiri wa vipaji vya mpira wa miguu vilivyosheheni nchini Brazil ili kukuza wachezaji wa Zanzibar hasa chipukizi, ikiwezekana kuwaleta magwiji wa soka wa taifa hilo akiwemo Edson Arantes Dos Nascimento (Pele) na wanasoka wengine mahiri.

Amewaomba wananchi wa Zanzibar kutumia fursa ya kuwepo ubalozi huo kwa kuanzisha ubia wa kiuchumi, kibiashara, michezo na utamaduni ili Zanzibar iweze kupiga hatua zaidi ya maendeleo.

Tafrija hiyo ilihudhuriwa pia na mawaziri mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mabalozi wadogo wanaofanya kazi hapa na wananchi wengine.

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

OKTOBA 12, 2018.