Halmashauri ya wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera imeendelea na kutekeleza shughuli za lishe ili kupambana na tatizo la udumavu mkoani humo.

Wakijadili kwa pamoja katika kikao kilichofanyika ndani ya Halmashauri hiyo, wajumbe wa kikao hicho wameeleza kuwa suala la udumavu si tu linaathiri ukuaji wa mtoto chini ya miaka 5 Bali pia linaathiri uwezo wa mtoto kufikiri, na kubuni hivyo kupelekea watoto kutofanya vizuri katika masomo yao na hata wanapokuwa watu wazima hushindwa kufanya maamuzi kulingana na umri na elimu zao hivyo kupelekea kutofikia malengo yaliyopangwa.

Afisa lishe katika halmashauri hiyo Bwana Desdery Karugaba amesema kuwa mikakati mbalimbali imepangwa na Halmashauri hiyo ili kuhakikisha suala la udumavu linakomeshwa kabisa.

Afisa lishe wa Halmashauri ya wilaya ya Bukoba Bwana Desdery Karugaba

Aidha Bwana Karugaba amesema ni muda sasa kwa walimu wa shule za msingi kuwa na mbegu zitakazo wasaidia katika kuhakikisha wanapata huduma za lishe mashuleni .

Kwa upande wake Kaimu Mganga wa Mkuu wa Halmashauri hiyo Dk. Bandioti Gavyole amesema kuwa shabaha kubwa ya kikao hicho ni kupunguza udumavu kwa watoto chini ya miaka 5, kuboresha huduma za lishe katika vituo vya kutolea huduma za afya, kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa na uzito pungufu na pia kwa wanafunzi.

Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Bukoba Dk. Bandioti Gavyole

Na Lydia Lugakila, Bukoba