Pamekuwepo na imani kwa wengi kwamba bundi anaponekana nyumbani kwa mtu ni lazima kuna mtu atakufa katika nyumba hiyo.

Hivyo imewapelekea watu wengi kuwa na hofu kubwa sana juu ya kiumbe hiki cha Mungu na hivyo kukihusianisha na nguvu za giza kwamba ni lazima ametumwa na mchawi ili kuchukua roho ya mtu.

UKWELI UPO HIVI:

Bundi ni aina ya ndege ambaye hula nyama na hufanya mawindo yao wakati wa usiku na kupumzika wakati wa mchana.

Bundi ana uwezo mkubwa sana wa kuvuta harufu ya mzoga kutoka mbali. Uwezo huu wa kunusa harufu unapita uwezo walionao binadamu.

Hivyo inapotokea katika nyumba fulani kuna mgonjwa mahututi ambaye seli za mwili wake zimeshaanza kufa lakini mapigo ya moyo bado yanafanya kazi; Bundi huweza kunusa harufu ya seli hizo, harufu ambayo binadamu hawawezi kuihisi, na hivyo huvutiwa kuisogelea kwa ajili ya kujipatia chakula, ila hataweza kuingia ndani kwa kuhofia binadamu. Kwa kawaida binadamu hafi mara moja, bali hufa hatua kwa hatua. Zinaanza kwanza kufa seli za mwili, baadaye ogani mbalimbali za mwili.

Ogani za mwisho kufa ni moyo ikifuatiwa na ubongo. Hivyo bundi anapoonekana kwenye nyumba yenye mgonjwa mahututi ni dalili kwamba mgonjwa huyo ameshaanza hatua za kufariki, na hivyo uwezekano wa mgonjwa huyo kufariki siku za karibuni ni mkubwa sana.

Inapotokea kwamba mgonjwa amekufa baada ya bundi kuonekana, tafsiri sahihi siyo kwamba kifo kimesababishwa na bundi bali ni kwamba dalili za kifo cha mgonjwa huyo zimetambuliwa na bundi.

Hivyo cha kufanya siyo kumtafuta mchawi bali ni kuzidi kumkabidhi mgonjwa huyo katika huruma ya Mungu kwa njia ya sala.

Hofu ya bundi kama kiumbe chenye nguvu za giza ipo zaidi Afrika. Ulaya hawana hofu hiyo. Wao humtazama bundi kama kiumbe cha Mungu, kiumbe cha ajabu, na hivyo huvutika kukaribia kwa njia ya utalii, utafiti na hata ufugaji.

Zipo mbuga za wanyama zinazofuga bundi. Sifa mojawapo ya bundi inayowavutia watalii wengi kumtazama ni ule uwezo wake wa kugeuza shingo kutoka mbele mpaka nyuma pasipo kuhitaji kugeuka kwa kiwiliwili chake.

 

Hivyo hatupaswi kuwaogopa, kuwachukia bundi ama kuongea vibaya juu yao. Hao ni viumbe vya Mungu kama walivyo njiwa, kondoo, v n.k. Wao ni kazi ya Mungu.

Hivyo kuongea vibaya juu ya bundi ni kuongea vibaya juu ya kazi ya Mungu na hiyo kumpa shetani nafasi ili hofu izidi kutawala miongoni mwa watu.

Kwa hiyo tunapowaona bundi tuna wajibu wa kumpa Mungu SIFA NA UTUKUFU Kwa Kuwa Uwezo Huu Umetoka Kwake.