Bunge limepitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba sita wa mwaka 2019, yanayohusisha kuweka adhabu kwa watu wanaotumia au kusambaza picha za maiti au wahanga wa ajali na kubadilisha muundo na majukumu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Jamii (SSRA).

Akiwasilisha muswada huo uliokuwa na mapendekezo ya marekebisho katika sheria tisa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi alisema mabadiliko hayo yanahusisha Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 iliyotungwa mwaka 1930 kwa lengo la la kuainisha adhabu kwa makosa mbalimbali.

Alisema tangu kutungwa kwa sheria hiyo, imerekebishwa mara 67 kupitia sheria mbalimbali na marekebisho ya sasa yanalenga kuongeza adhabu ya faini kwa makosa chini ya kifungu cha 29, ili kuondoa adhabu zilizopitwa na wakati kutokana na hali ilivyo sasa.

“Kifungu kipya cha 162 kinapendekezwa kuongezwa ili kutoa adhabu kwa watu wanaotumia na kusambaza picha au video za maiti, waathirika wa majanga na matukio ya kutisha yanayohatarisha amani au kuingilia utu wa mtu,” alisema.

Katika mabadiliko hayo, adhabu zimebadilishwa katika Ibara ya 29 kutoka Sh 100 iliyokuwa ikisomeka awali na kufikia Sh 50,000 kwa makosa tofauti ambapo watuhumiwa wanaweza kutozwa hadi zaidi ya Sh 1,000,000.