WAZIRI wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Maudline Castico, amesema serikali haikuwa tayari kugeuzwa kuwa uchochoro wa ajira mbaya za utumikishaji watoto kama zinazofanya nchi nyengine.

Hayo aliyasema wakati akizungumza na Zanzibar Leo,katika nyumba ya kulelea watoto yatima Mazizini mjini Unguja, kufuatia kuwepo tukio la mtoto wa miaka 10 aliyekutwa akitumikishwa na watu waliomchukua kwa ajili ya kumsomesha.

Waziri huyo alisema watu hao wameenda kinyume na sheria za kumlinda mtoto aliye chini ya uangalizi wa wazee wake kwa kumfanyisha kazi huku wakimpa mateso ikiwemo kipigo kizito kwa kutumia waya.

Alisema inasikitisha kuona watu waliofanya ukatili huo wanaufanyia Zanzibar, ikiwa tayari serikali imepiga marufuku ya utumikishaji wa watoto majumbani.

“Sisi kama serikali tunalaani tukio hili na hatutavumilia kuona Zanzibar inageuzwa kigezo cha vitendo vya utumikishaji wa watoto kama yalivyo mataifa mengine duniani, hatutaacha tabia hii itokee hapa visiwani kwetu, tutawalinda watoto na mambo maovu,” alisema.

Alisema Zanzibar inapata kesi nyingi za watu kunyanyaswa nje ya nchi kwa wanaotumikishwa majumbani na ndio maana serikali imeamua kuingilia kati suala hilo kwa kuandaa mazingira bora kwa wanaotaka kufanya kazi za majumbani nje ya nchi.

Kutokana na hilo Waziri Castico, alisema kesi ya mtoto huyo, serikali itahakikisha inaisimamia ipasavyo ili kuona wazee waliomsababishia vitendo vya ukatili kwa kumpiga waya hadi kumchana sehemu za mwili wake.

Hata hivyo, Waziri huyo, alionya watendaji wanaosimamia kesi hiyo, kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria kwa vile mtoto aliyetendewa tukio hilo ana uwezo wa kujieleza.