CHAMA cha Mapinduzi Mkoa wa Magharibi Unguja kimesema kina matarajio ya kufanyika kwa ufanisi uchaguzi wa Chama na jumuiya ndani mkoa huo baada ya kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizojitokeza katika mchakato huo hivi karibuni.

Akizungumza Katibu wa Mkoa huo, Bi. Aziza Ramadhan Mapuri mara baada ya kufanya ziara fupi katika  Wilaya za Dimani na Mfenesini na kuzungumza na wajumbe wa Kamati za Sekreterieti za wilaya 6hiyo kwa lengo la kufanya tathimini ndogo juu ya maendeleo na kasoro zilizopo katika  uchaguzi huo.

Amesema ziara hiyo imekuja baada ya wanachama kutojitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi kwa  ngazi za mashina na matawi ya jumuiya kutokana na kuwa na hofu iliyotokana na kutoelewa marekebisho ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977, juu ya kipengele cha kinachosema kazi za muda wote kwa baadhi ya nafasi zinazogombewa.

Alisema wanachama wengi waliokuwa na nia ya kuchukua fomu walitawaliwa na hofu ya kuwa endapo watajitokeza kuwania nafasi za ngazi hizo watakuwa hawana fursa za kugombea nafasi zingine katika ngazi za juu.

Aidha Katibu huyo alifafanua kwamba nafasi zilizotajwa kuwa ni za muda wote ni zile za kiutendaji zikiwemo za Katibu na Mwenyekiti lakini zingine zilizobaki zinaruhusiwa kushika nafasi zaidi ya moja na kwa ngazi tofauti.

Pia alieleza kwamba chanzo cha kuwepo kwa ziara hiyo ni baada ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadalla kubaini mapungufu katika mchato huo na kuagiza ngazi husika za chama na jumuiya kutoa elimu na maelekezo ya kina juu ya changamoto hizo kwa viongozi wa ngazi zote ili nao wawaelimishe wanachama katika maeneo husika.

” Tunatarajia kuwa baada ya kuongezwa muda wa uchaguzi wanachama wetu wengi watajitokeza zaidi kuchukua fomu ili kupata viongozi wengi.”, alisema Bi. Aziza.

Hata hivyo alipongeza maamuzi ya busara na hekima ya kujenga chama yaliyofikiwa na Naibu Katibu Mkuu huyo kwa kuongeza muda wa uchukuaji wa fomu ambapo kwa mujibu wa taarifa ya awali uchaguzi wa ngazi za chama ulikuwa ufanyike April 17 hadi 31 mwaka huu lakini kwa sasa utafanyika April 25 hadi 31 mwaka huu.

Kwa upande wa uchaguzi huo kwa ngazi ya Jumuiya za chama utafanyika Juni 18 hadi 22 mwaka, na matarajio ya mkoa huo ni kuona muda uliobaki unatumiwa vizuri na Wanachama wa chama hicho kwa kuchukua fomu kwa wingi ili kupata viongozi na watendaji wenye sifa na vigezo vya kukiimarisha chama na jumuiya.