Kukamatwa, kushikiliwa kwa muda na kuhojiwa kabla ya kuachiwa kwa Wasaidizi wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika kumeibua mgongano kati ya Jeshi la Polisi na chama hicho

Mgongano umeibuka baada ya pande hizo kutaja eneo tofauti la tukio na sababu za kukamatwa kwa watu hao ambao ni Afisa Habari wa CHADEMA na Msaidizi Binafsi wa Mnyika, Abdulkarim Muro na dereva wa Mnyika, Said Haidan

Wakati Polisi kupitia kwa Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Jumanne Muliro inadai Watu hao walikamatwa kwenye nyumba moja jirani na Hoteli ya Paradise eneo la Mahina, CHADEMA wanadai ukamataji ulifanyika ndani ya hoteli hiyo

Pande hizo pia zimetofautiana sababu za ukamataji kwa Polisi kudai ulitokana na taarifa ya Raia wema kuhusu kuwepo wa watu wanaohisiwa kuwa ni wahalifu wakati CHADEMA wanadai walikamatwa kama sehemu ya kumsaka John Mnyika aliyekuwa jijini Mwanza kwa mapumziko

Kamanda Muliro amesema, Maafisa hao katika mahojiano ya awali walikataa kutoa utambulisho wao na wamefika maeneo hayo kufanya shughuli gani, walipelekwa Polisi kisha kutoa ushirikiano na Polisi kujiridhisha na kisha kuwaachia