Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa taarifa za Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama na Waziri Mkuu Mstaafu, Mzee Frederick Sumaye kupata msiba wa kufiwa na Mama yake Mzazi, Bi. Elizabeth Gisa Sumaye, aliyefariki Jumatano, Novemba 7, 2018 kijijini kwake Endasaki, Hanang, mkoani Manyara kwa ugonjwa wa moyo na mapafu.

Kufuatia msiba huo, CHADEMA kupitia Katibu Mkuu wa Chama, kinatoa salaam za pole na rambirambi kwa Familia ya Mzee Sumaye, ndugu na jamaa kwa kufiwa na Mama na Bibi, akiwa ni moja ya nguzo muhimu katika familia na maisha yao. Mwenyezi Mungu awapatie faraja na kuwajalia nguvu wakati huu wa majonzi makubwa ya kuomboleza msiba huo.

Chama kitaendelea kushirikiana na Familia ya Mzee Sumaye kutoa taarifa kuhusu msiba huo ambao shughuli zake, ikiwemo mazishi, zitafanyikia kijijini Endasaki, Hanang, Manyara.