Chadema kujadili ushauri wa wazee kuhusu kumvuta Maalim Seif

Uongozi wa Chadema umesema utaanza kujadili ushauri wa baraza la wazee la chama hicho, kuhusu kumvuta Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif kuwania urais kupitia Chadema.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Septemba 12, Katibu Mkuu wa Chadema Vicent Mashinji amesema ni muhimu kufuata ushauri na kuufanyia kazi.

“Wale ni wazee walitoa maoni yao hivyo chama kitajadili na kutoa tamko,” amesema.

Jana Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema, Hashimu Juma alisema  CUF ikipasuka Zanzibar, Chadema wanachukua nafasi na kumkaribisha Maalim Seif na wabunge wake Chadema.

“Lengo la upinzani ni kuhakikisha maendeleo yanakuwepo nchini hivyo kwa kuwa CUF ipo katika mgogoro Seif anaweza kuhamia Chadema kwenye nafasi ileile na atapata nafasi ya kuwania urais,”alisema Juma.