Wananchi wa Kijiji cha Umbuji Wilaya ya Kati Unguja wamesema kuwa
udogo wa jengo la kituo cha Afya Kijijini hapo ni moja  ya changamoto
inayowakabili katika upatikanaji wa huduma za afya.

Wakizingumza na waandishi wa habari kijijini hapo,walisema kituo hicho
hakiendani na hadhi ya kuwahudumia wananchi wa  jimbo la Umbuji  katika utoaji wa huduma.

Khatib Abdalla mkaazi wa kijiji hicho,alisema kituo hicho kimejengwa
kwa ajili ya huduma za afya ya Mama na Mtoto lakini kutokana na
ukosefu wa kituo cha afya imelazimika kituo hicho kutoa huduma kwa
watu wote.

“Hiki kituo ni kidogo sana hao akinamama wenyewe na watoto hakiwatoshi hivyo tunaiomba serikali itujengee jengo jengine kwa ajili ya kituo cha afya kwa watu wote”alisema.

Khatib alisema mkusanyiko wa akinamama wajawazito na watu wengine
ambao hupatiwa huduma za afya kituoni hapo ni changamoto pia kwa
akinamama kwani wanahitaji eneo maalum ili kuweza kufichiwa siri zao.

“Tunashukuru mradi wa uwajibikaji wa (PAZA)ambao unatekelezwa na chama
cha waandishi wa habari za maendeleo (WAHAMAZA) kushirikiana na
taasisi ya msitu wa Ngezi (NGERENACO)  tumekuwa tukipaza sauti zetu
kwa kueleza changamoto mbalimbali ambazo baadhi zimefanyiwa kazi
tunaomba na hili la kituo cha afya lifanyiwe kazi”alisema.

Alieleza kuwa wanapoeleza maradhi yanayowasumbua husikika na watu
wengine hivyo ni vyema kutengewa eneo la faragha ili kuweza kueleza
matatizo yao bila ya kuona aibu.

“Wakati mwingene Mama mjamzito anavua nguo ili kuweza kumuonesha
daktari ugonjwa unaomsumbua na akinababa tupo hapo hapo hivyo hailetipicha nzuri hasa huku vijijini”
alisema.

Nae Rashma Shaaban mkaazi wa Pagali ambaye alifika kituoni hapo kwa
ajili ya kupata huduma ,alisema kituo hicho kwa sasa ni kidogo na
hakikidhi mahitaji ya akinamama na watoto wanaofika hapo kufuata
huduma.

‘’Hichi kituo ni kidogo lakini pia hakina madaktari wa kutosha unakuja hapa unachukuwa muda mrefu kwa ajili ya kupata huduma za uchunguzi wa afya ya mtoto’’alisema.

Kwa upande wake mkuu wa kituo hicho ambae hakutaka kutajwa jina lake
alikiri udogo wa kituo hichona upungufu mkubwa wa madaktari na
wahudumu katika hospitali hiyo kulingana na mahitaji ya wananchi.

‘’Tupo wafanyakazi watano tu katika kituo hichi ambacho kinatoa huduma za afya kwa wananchi takriban 7,000 kwa mwezi’’alisema.