Direct Aid wakamilisha mradi wa maji Kianga

Wananchi wa wa Shehia ya Kianga (Rafia) wametakiwa kuhakikisha wanatunza miradi mbali mbali ya maji inayozinduliwa ili kunufaika baadae na vizazi vyao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa miradi ya maji ilodhaminiwa na Shirika la Direct Aid Sheha wa Shehia hiyo Juma Issa Juma amesema wao kama serikali ya mitaa ipo tayari kupokea wafadhili wowote wenye nia njema na wana lengo zuri kufadhili miradi mbali mbali.

Hata hivyo Sheha huyo amesema bado kuna maeneo mengine katika shehia hiyo kuna changamoto za maji ambazo zinahitaji kutatuliwa kama vile za Chemani, wete, domoni, na Kianga meli nane.

Kwa upande wake Mkuregenzi wa Shirika la Direct Aid Aiman Kamal Din amesema bado wanaendelea na mpango huo kwenye shehia hiyo ya Kianga baada ya kumaliza ujenzi wa kisima kikubwa kwenye eneo la Msikiti na Skuli ambazo kitagawa maji kwenye baadhi ya maeneo ya Shehia hiyo.

Kwa upande mwengine Aiman Kamal Din ameipongeza serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kulipa nafasi shirika la Direct Aid kwa kuendelea kudhamini miradi mbali mbali ndani ya visiwa vya Zanzibar.

Kwa upande wao wananchi wa shehia hiyo wamelipongeza shirika hilo kwa kuendelea kudhamini miradi ndani ya Kijiji cha Kianga kama vile ujenzi wa misikiti na na vyuo mbali mbali.