MAHAKAMA Kuu ya Zanzibar imepiga marufuku shughuli zote za muziki katika Hoteli ya Ngalawa iliopo eneo la Kihinani Mkoa wa Mjini Magharib Unguja.

Kwa mujibu wa hukumu ya Mahkama Kuu katika kesi ya madai namba 72 ya mwaka 2016, katika uamuzi wake imetoa amri ya kusitisha upigaji muziki hadi hapo ombi hilo litakaposikilizwa pande zote mbili.

Mrajis wa Mahkama kuu ya Zanzibar katika barua yake kwenda kwa Hoteli ya Ngalawa ya Juni 13 mwaka huu, uongozi wa Hoteli hiyo umetakiwa kutekeleza amri hiyo mara moja .

Nakala ya uamuzi huo imepokelewa kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Bububu , Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi na Shehe wa Shehia ya Chuini kwa ajili ya utekelezaji wa amri ya Mahkama .

Kesi hiyo ya madai imefunguliwa na Hakuna Matata Beach Lodge Limited, Chuini Zanzibar Beach Lodge Limited na Mangrove Beach Hotel Limited dhidi ya Ngalawa Beach Resort Hotel Limited.

Agizo hilo ni la pili kutolewa na Mahkama Kuu ya Zanzibar ambapo mara ya mwanzo lilitolewa mwaka jana lakini uongozi wa hoteli hiyo ulipuuza kutekeleza na Meneja wake kupewa adhabu ya kutumikia kifungo cha mwezi mmoja Chuo cha Mafunzo Zanzibar kwa kudharau Mahkama.

Amri hiyo ya Mahkama imekuja wakati ambapo wananchi wa eneo hilo la Chuini wamelalamikia uongozi wa Hoteli hiyo kupiga mziki kwa sauti na kusababisha kero kwao .

Baadhi ya wananchi wa maeneo hayo wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema kelele za muziki ikiwemo disko limekuwa kero kwa watoto wao kukosa utulivu wa kusoma hasa kipindi wanapojitaarisha na mitihani ya taifa.

“Hapa kuna kelele nyingi , tumechoka kwa kweli , tunaiomba Serikali kufungia ukumbi huu wa disko  la chaza kwani hata vijana wetu hawana utulivu wa kusoma na hata wanaweza kuharibika kwa kujiingiza katika mambo ya starehe, walisema wananchi hao.

Khamis Faki anaeshi katika eneo hilo alisema wamechoka na kelele za ngoma zinazopigwa kwa sauti kubwa bila kujali hali zao hivyo  wameiomba Serikali kuufungia ukumbi wa disko ili kupata utulivu.

Pia Haji Ramadhani  mkaazi wa Chuini amesema yeye na wenziwe wa Shehia hiyo wamefurahika na uamuzi huo kwa sababu changamoto kubwa zilikuwa zikiwakabili kwa kukosa utulivu wakati wa usiku kelele nyingi .

Vile vile wagonjwa, watoto wanakosa utulivu wakati wa usiku kwani kelele zinakuwa nyingi mitaani hivyo wamefurahika na uamuzi huo.