Mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha Mapinduzi Dr Hussein Ali Mwinyi ameahidi kuweka mikakati mikubwa ya kuboresha makusanyo ya serikali ya Mapinduzi kwa nia ya kuinua maisha ya wazanzibari.

Dr Mwinyi pia amesema mikakati hiyo ya kuboresha makusanyo ya mapato ya serikali itasaidia kutimiza ahadi zake alizoahidi katika kipindi hiki cha kampeni cha kuomba kuchaguliwa kuwa  Rais wa awamu ya nane ya Zanzibar.

Mgombea huyo wa urais wa Zanzibar ametoa ahadi hiyo  mara tu baada ya kuzungumza na mabalozi wa nyumba kumi katika mkutano uliofanyika leo kwenye ukumbi wa chuo cha kiislam wilaya ya micheweni mkoa wa kaskazini.

Baadhi ya miradi iliyoahidiwa na mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kupitia ccm  ni kujenga bandari za kisasa unguja na pemba,kuuboresha uwanja wa ndege wa pemba,kusambaza maji kwenye maeneo ambayo bado yanakabiliwa na upungufu wa huduma pamoja na kujenga matanki makubwa ya kuhifadhi maji na kuziwekea lami bara bara za ndani.

Pia kwenye ahadi hizo Dr Mwinyi ameahidi kuboresha bandari ndogo ndogo kwa ajili ya kuikuza sekta ya uvuvi,kutoa mitaji kwa wajasiriamali,kujenga hospitali ya rufaa ya kisasa,kuongeza ajira ya madaktari bingwa na walimu wa masomo ya sayansi na hisabati.

Katika  mazungumzo mafupi na vyombo vya habari wilayani micheweni pia mgombea huyo wa urais ameahidi kuiendeleza ardhi ya Zanzibar iliyopo wilayani Bagamoyo ambayo serikali ya muungano iliitoa tangu wakati wa uongozi wa Marehemu Aboud Jumbe Mwinyi.

Kuhusiana na uchaguzi mkuu wa tarehe ishirini nane mwezi huu Dr Hussein Ali Mwinyi amewaomba wanaccm wote kupitia kwa mabalozi kutorudia makosa ambayo yamekuwa yakisababisha chama cha mapinduzi kupoteza kura nyingi.

Tatizo jingine lililotajwa na Dr Mwinyi ambalo limekuwa likikipotea kura chama hicho ni watu kuogopa kwenda kwenye vituo kutokana na woga.amewataka wanaccm kisiwani pemba kutokuwa na hofu kwakuwa vyombo vya usalama vimeandaa ulinzi wa kutosha.

Vile vile  ametaja sababu ya kuwa na mawakala dhaifu katika kusimamia kwenye chaguzi zilizopita kuwa ni chanzo kingine ambacho kimekuwa kikissababisha  ccm kupoteza kura nyingi hivyo kuwaomba kuweka wasimamizi wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo.

Aidha Dr Hussein Ali Mwinyi amewaahidi mabalozi wote wa pemba kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwake mjini Unguja kama atachaguliwa kuwa Rais wa Visiwa hivyo.Kisiwa cha Pemba kinakadiriwa kuwa na mabalozi wa nyumba kumi wapatao mia tisa.