RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa barabara zinafungua milango na kuleta manufaa katika ukuaji na maendeleo ya uchumi na kijamii.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo jana katika ufunguzi wa barabara ya Ole hadi Kengeja yenye urefu wa kilomita 35, hafla iliyofanyika huko katika viwanja vya skuli ya Kengeja, Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba.

Viongozi mbali mbali walihudhuria katika hafla hiyoakiwemo Mama Mwanamwema Shein, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Naibu Katibu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi, Mawaziri pamoja na viongozi wa vyama vya siasa, Serikali na wananchi,

Alisema kuwa ujenzi wa barabara unaimarisha makaazi ya wananchi kwani walio wengi huvutika kujenga karibu na maeneo ya barabara ambapo pia shughuli za maendeleo ya biashara, kilimo, uvuvi na nyenginezo nazo huimarika.

Serikali ya Awamu ya Saba imejitahidi kuweka mfumo wa barabara katika hali nzuri hivyo, ni wajibu wa Taasisi nyengine zinazohusika na usafiri na usafirishaji pamoja na usalama wa abiria na mizigo kushirikiana pamoja kuona kuwa ajali za barabarani zinapungua.

Alitumia fursa hiyo kuziagiza Mamlaka zinazohusika kuweka alama za usalama barabarani ili ziwaongoze madereva na wapita njia katika kuzitumia barabara vizuri kwa usalama wao na vyombo vinavyoendeshwa.

Alisema kuwa kujenga barabara ni gharama lakini ikiwa zitatumika vyema na kupata matunzo mazuri gharama hizo zinafidiwa na ukuaji wa wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja, jamii na nchi kwa jumla.

“Tumeweza, hatimae tumejenga sisi wenyewe  na mkopo wa Benki ya Kimataifa ya Nchi zinazotoa Mafuta kwa wingi (OFID) haukutosha tukaongezea wenyewe hivyo, wajue kama na sisi wenyewe tuna uwezo mkubwa”, alisisitiza Rais Dk. Shein.

Akitoa maelezo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Mustafa Aboud Jumbe alisema kuwa ujenzi wa barabara hiyo yenye kilomita 35 unajumuisha Wilaya mbili za Chake Chake na Mkoani na kupita katika Shehia 15.

Pia, alisema kuwa barabara hiyo ina upana wa mita 7.5 na imejengwa kwa kiwango cha lami ya moto na ina uwezo wa kutumiwa na gari yenye uzito wa tani 10 ambayo ina madaraja 16 na culvert ndogo ndogo 118 pamoja na miundombinu ya kupitishia huduma za kijamii ikiwemo mabomba ya maji.

Alieleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo umefanywa na Wizara ya Ujenzi, mawasiliano na Usafirishaji kupitia Idara yake ya UUB ambayo sasa ni Wakala wa Barabara chini ya Usimamiazi wa Kampuni ya Kizalendo ya KAPSEL kutoka Dar es Salaam.

Alisema Ujenzi huo umefanywa kupitia mkopo wa Benki ya Wanachama wa Nchi zinazotoa mafuata kwa wingi Duniani (OFID) ikishirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo hadi kukamilika kwake mradi huo umegharimu TZS Bilioni 30.935.

Alisisitiza kuwa kati ya fedha hizo mkopo kutoka OFID umechangia TZS Bilioni 24.2 na SMZ imechangia TZS Bilioni 6.735.

Nao wananachi walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuijenga barabara hiyo ambayo itakuwa ni kichocheo cha uchumi na maendeleo yao.