Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi  wa Zanzibar kuendelea kuidumisha hali ya amani na utulivu ambayo ndio msingi wa mafanikio yanayoendelea kupatikana hivi sasa na yatakayopatikana hapo baadae.

Dk. Shein ameyasema hayo leo katika risala yake ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2019 aliyoitoa kupitia vyombo vya habari, Ikulu mjini Zanzibar.

Dk. Shein amesema kuwa katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya mwaka 2018 mafanikio makubwa yamepatikana ambayo yamechangiwa na kuwepo kwa amani, mshikamano, umoja na mapenzi yaliopo.

Katika risala yake hiyo Dk. Shein alieleza kuwa hali ya amani, umoja na mshikamano uliopo nchini ni jambo muhimu linalowavutia Washirika wa maendeleo ambao wanaridhika na jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ndio maana wanaiunga mkono katika mipango yake ya maendeleo.

Amesema kuwa hapana shaka kwamba iwapo amani, usalama na utulivu vitadumishwa na kufanya kazi kwa bidii Washirika wa Maendeleo watakuwa pamoja na Zanzibar katika kuisaidia ili kuweza kutekeleza malengo yaliyopangwa.

Rais Shein alitoa shukurani kwa wananchi wote kwa kuunga mkono juhudiza serikali za kuiletea maendeleo Zanzibar na kueleza kuwa moyo wao huo wa umoja na mshikamano umewezesha kuimarisha vizuri hali ya uchumi wa Zanzibar.

Hata hivyo, Dk. Shein alitoa shukurani nyingi kwa wananchi wote kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuiletea maendeleo Zanzibar ambapo moyo wao huo wa umoja na mshikamano umewezesha kuimarisha vizuri hali ya uchumi wa Zanzibar.

“Tukiwa tunaukaribisha mwaka mpya wa 2019, nachukua fursa hii kwa niaba ya wananchi wote  wa Zanzibar kuwashukuru kwa dhati  Washirika wetu wa Maendeleo kwa kuendelea kutuunga mkono, tunathamini mikopo, misaada na ushauri tulioupata kutoka kwao”, alisema Dk. Shein.