Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Zanzibar si mwanagenzi wa viwanda hivyo kuanzishwa kwa  kiwanda kipya cha nguo cha Basra Textile Mills Ltd kutairejesha Zanzibar katika medani ya viwanda.

Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kuweka jiwe la msingi la  Kiwanda kipya cha nguo cha Basra Textile Mills Ltd, kilichopo Chumbuni, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni hafla ya mwisho ya uwekaji wa mawe ya msingi wa miradi katika uongozi wake akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Rais Dk. Shein alitoa shukurani maalum kwa mwekezaji na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Basra Textile Mills Ltd Ahmed Osman kwa uwamuzi wake wa kuja kujenga kiwanda cha ushoni na kutengeneza nguo hapa Zanzibar.

Alieleza kuwa hatua yake hiyo ni katika kuziunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha sekta ya viwanda kama ilivyoelezwa katika ibara ya 84 ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Alisema kuwa Kampuni hiyo ina uwezo mkubwa na kiwanda hicho kitakuwa ni cha mfano katika ukanda wa Afrika Mashariki na matarajio kiwanda hicho ni kuzinduliwa mnamo Januari mwakani katika sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Januari 1964.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka 10 ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, juhudi za kuimarisha sekta ya viwanda zilizochukuliwa, zimezaa matunda ambayo baadhi yake ni kuanzishwa kwa kiwanda hicho cha nguo cha Basra.

Alisema kuwa kiwanda hicho ni matokeo ya juhudi za Serikali za kuimarisha sekta ya viwanda ambapo mradi huo ni mkubwa wa kimkakati ambao utatoa fursa za ajira kwa wananchi wengi hatua kwa hatua.

Alisema kuwa ajira 1,600 zitakazotolewa katika kiwanda hicho ni miongoni mwa ajira 300,000 anazozielezea mgombea wa Urais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi katika mikutano ya kampeni za CCM unguja na Pemba.

Mapema akisoma risala ya muekezaji Saleh Suleiman Hamad alisema kwamba Mradi wa Basra Textile Mills Ltd ni mradi uliosajiliwa Zanzibar na kuanzishwa kupitia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji (ZIPA) katika mwaka 2019.

Alisema kuwa Mradi huo umepangwa kutekelezwa kwa awamu tatu na kuzalisha bidhaa za aina mbali mbali za vitambaa na mavazi ambapo hadi kukamilika kwa awamu zake tatu unatarajiwa kugharimu kiasi cha TZS Bilioni 115.50 na kuajiri wafanyakazi wapatao 1,600.

Alisema kuwa mradi huo ukikamilika utaweza kuzalisha kiasi cha mita 250,000 za vitambaa kwa siku, ambayo ni sawa na mita milioni 7.5 kwa mwezi.

Sambamba na hayo, alizitaja bidhaa zinazotarajiwa kuzalishwa kuwa ni pamoja na vitenge, kanga, mashuka ya vitanda, mapazia, vitambaa vya mashati, vikoi, madira ya akina mama, sare za aina mbali mbali, vitambaa vya suti na kadhalika.

Alisisitiza kwamba masoko ya bidhaa za mradi huo ni nchi za Afrika Mashariki, Afrika ya Kati, Kusini mwa Afrika na hatimae Ulaya na Marekani.