Dkt. Shein atuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Indonesia

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Joko Widodo kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea katika kisiwa cha Lombok ambacho ni maarufu kwa utalii kilicho katika maeneo ya karibu na kisiwa cha Bali.

Katika salamu hizo za rambirambi, Rais Dk. Shein alieleza kuwa tetemeko hilo la ardhi limewaua watu wapatao 100 na kuwabakisha wananchi wapatao 20,000 ambao hawana makaazi.

Salamu hizo ziliendelea kuweleza kuwa niaba ya wananchi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na yeye mwenyewe binafsi, Rais Dk. Shein anatuma salamu za  rambi rambi kwa serikali, familia pamoja na ndugu jamaa na marafiki wa nchi ya Jamhuri ya Indonesia kufuatia tukio hilo kubwa la kusikitisha.

Salamu hizo ziliongeza kuwa wananchi wa Zanzibar pamoja na wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla wako pamoja na ndugu zao wa Indonesia hasa wale wanaoishi katika kisiwa cha Lombok ambao wameathiriwa na tukio hilo kubwa la kuhuzunisha.

Aidha, salamu hizo za rambirambi alizozitoa Dk. Shein alimuomba Mwenyezi Mungu kuendelea kuwapa afya njema na kupona kwa haraka wale wote waliopata majeraha

Salamu hizo za rambirambi alizozituma Rais Dk. Shein alimuomba MwenyeziMungu awape moyo wa subira ndugu, jamaa, marafiki na wanafamilia wote wa Marehemu pamoja na wananchi wa  Jamhuri ya Indonesia katika tukio hilo la  kuhuzunisha.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alimuomba Mwenyezi Mungu kuzilaza roho za marehemu mahala pema peponi. Amin.

Tukio hilo limetokea siku ya Jumaapili ya Agosti 5 mwaka 2018 ambapo tetemeko hilo lenye nguvu ya 7 kwenye vipimo vya Richter pia liliharibu vibaya miundombinu ya umeme na barabara sambamba na nyumba za maakaazi ya wananchi, ofisi pamoja na nyumba za ibada.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar