Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  ameungana pamoja na Wapiganaji wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama waliovyoshiriki katika Maadhimisho ya sherehe za kutimiza miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika chakula maalum cha mchana alichowaandalia.

Chakula hicho maalum cha mchana aliwaandalia kutokana na ushiriki wao kwenye sherehe hizo za miaka 55 ya Mapinduzi zilizofanyika Januari 12 mwaka huu 2019 huko katika uwanja wa Gombani Chake Chake Pemba.

Hafla hiyo ya chakula maalum ilifanyika leo katika  Kambi ya Mafunzo ya Jeshi ya Chukwani ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Mawaziri, Manaibu Mawaziri na viongozi wengine pamoja na Wapiganaji wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika shukurani zake Dk. Shein kwa Wapiganaji hao zilizotolewa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi Gavu alitoa pongezi kwa Wapiganaji hao kwa kushiriki kikamilifu katika sherehe hizo adhimu.

Alieleza kuwa hatua hiyo ya Dk. Shein ya kuwaandalia chakula maalum cha mchana ni utamaduni aliouweka kila mwaka baada ya kumaliza sherehe hizo ambayo inaonesha wazi jinsi alivyokuwa na upendo pamoja na imani kubwa na wananchi wote anaowaongoza.

Hivyo,  Waziri Gavu alisisitiza haja kwa Vikosi hivyo vya Ulinzi na Usalama kuendelea kutimiza wajibu wao wa kulinda amani, utulivu na mshikamano ambapo pia, alitumia fursa hiyo kutoa pongezi maalum kwa ushiriki wao mzuri katika sherehe hizo.

Waziri Gavu alitoa shukurani za dhati kwa vikosi hivyo kwa kuazimisha kwa hali ya juu kilele cha miaka 55 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.

Waziri Gavu alisema kuwa gwaride hilo lililovutia sana lilikuwa ni kielelezo cha kutosha cha Mapinduzi ya Januari 12.1964 yaliyowakomboa Wazanzibari wote ambayo yataendelea kulindwa, kuenziwa na kutunzwa daima.

“ Imani ya kiongozi mwema siku zote haitafutwi kwenye jarida bali inatafutwa katika nafsi na nyonyo za watu anaowaongoza……..na sote tunaona jinsi ya upendo ulionao kwa wananchi wa Zanzibar na Tanznia nzima kwa jumla”.

“ …..hongereni sana sana sana Vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama kwa kazi kubwa mliyoifanya katika kilele cha miaka 55 ya Mapinduzi yetu ”,alisisitiza Waziri Gavu.

Aidha, alitoa shukurani kwa Wapiganaji wote pamoja na viongozi wao kwa kufanikisha kilele cha sherehe hizo na kusisitiza haja kwa vikosi hivyo kuendelea kusimamia amani, utulivu na mshikamano hatua ambayo itawapelekea viongozi wengine kutekeleza majukumu yao ya kuwaletea maendeleo wananchi kwa ufanisi mkubwa.

Nae Kaimu Brigedi Kamanda 101 KV Zanzibar Kanal Salum Serengo Mugoba alitoa shukurani na pongezi kwa Dk. Shein kwa kuendelea kuvijali vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na kuendeleza utamaduni wake huo aliouweka kwa kila mwaka mara baada ya sherehe za Mapinduzi ambapo Dk. Shein huwandalia chakula maalum cha mchana Wapiganaji hao na kula nao pamoja.

Kanal Mugoba alieleza kufarajika kwao na hatua hiyo ya Dk. Shein na kutoa pongezi na shukurani kwa niaba ya Wapiganaji wote walioshiri katika hafla hiyo adhimu.

Ni utamaduni aliouweka Dk. Shein wa kuwaandalia chakula cha mchana Vikosi vya Ulinzi vinavyoshiriki katika gwaride la sherehe za Mapinduzi pamoja na vijana na Wanafunzi ambao hushiriki sherehe hizo kwa kila mwaka ambapo hapo jana aliwaandalia vijana na Wanafunzi  chakula hicho huko katika Makao Makuu ya KVZ, Mtoni mjini Zanzibar.

Katika hafla hiyo pia, Kikundi cha Taarab cha Taifa kilitumbuiza pamoja na Grassbanda ya JWTZ.

Rajab Mkasaba, Ikulu

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk