Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema ujenzi wa jengo jipya la Abiria (Terminal III), katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume unapaswa kwenda sambamba na utoaji wa huduma bora kwa wasafiri.

Dk. Mwinyi amesema hayo leo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, wakati alipolitembelea Jengo jipya la Abiria (Terminal III) lililo katika hatua za mwisho kukamilika ujenzi wake.

Amesema ujenzi wa jengo hilo umefanywa ili kuimarisha upatikanaji wa huduma bora kwa wasafiri, hivyo akawataka wasimamizi wa ujenzi kuhakikisha kasoro mbali mbali zilizopo katika jengo hilo zinarekebishwa ili kuwepo utoaji mzuri wa huduma.
 

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ameridhishwa na hatua iliofikiwa ya ujenzi huo na kuwataka wasimamizi wa ujenzi kurekebisha mapungufu madogo madogo ili kuwa na uwanja wa kisasa na kuepuka hali iliyopo katika jengo la zamani.
 
Aliyataja maeneo yanayohitaji kushughulikiwa kuwa ni pamoja na kuongeza vizimba vya Uhamiaji, eneo la ukaguzi wa mizigo pamoja na kuongeza mashine kwa watendaji wa masuala ya‘Custom’.

Dk. Mwinyi aliwataka wasimamizi wa ujenzi huo kuhakikisha kunakuwepo mabango yanayoainisha taarifa za safari za ndege,kama ilivyo katika viwanja vyote vya Kimataifa Duniani.

This image has an empty alt attribute; its file name is image-992.png

Aidha, aliwataka kukamilisha hatua mbali mbali zilizobaki mbele ya jengo hilo, ikiwemo upandaji wa majani, ujenzi wa uzio na barabara ili kuupa haiba Uwanja huo.