Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameihakikishia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Saharawi kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar itaendelea kushirikiana na Taifa hilo pamoja na wananchi wake.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Saharawi  katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mahayub Buyema Mahafud, aliyefika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Jamhuri ya Muungano ikiwemo Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano wa kidugu uliopo kati ya pande mbili hizo na kuahidi kuwa utaendelea kuimarishwa

Aliongeza kuwa katika kuhakikisha uhusiano na ushirkiano unaimarika zaidi kati ya pande mbili hizo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano wake mkubwa kwa Balozi huyo ili aendelee kufanya kazi zake vyema hapa nchini.