Mbunge wa Tarime Mjini,  Ester Matiko amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti baada ya kupata kura 44 akimshinda mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche aliyepata kura 38.Heche ndio alikuwa mwenyekiti wa Kanda hiyo tangu mwaka 2014.

Akitangaza matokeo hayojana Jumapili Desemba Mosi, 2019 msimamizi wa uchaguzi huo, Boniface Jacob ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Ubungo jijini Dar es salaam amesema wajumbe 85 walipiga kura.

Katika uchaguzi huo, Gimbi Masaba alichaguliwa kwa kura 45 kuwa makamu Mwenyekiti huku Maendeleo Makoye akishinda uweka hazina kwa kupata kura 42.

Wajumbe wa mkutano huo walilazimika kurejea kupiga kura katika nafasi ya mweka hazina baada ya mshindi kutopatikana katika awamu ya kwanza ya kura.

Wagombea katika nafasi hiyo walikuwa mbunge wa Viti maalum,  Catherine Ruge aliyekuwa akitetea nafasi aliyokuwa akiishikilia, Meshack Kajala na Percaline Sanya.