Ghala ya tume ya uchaguzi yateketea kwa moto

Moto ambao chanzo chake hakijafahamika umeteketeza ghala ya tume ya uchaguzi nchini Congo.

Inasemekana kuwa Mashine zaidi ya 7000 za kura na vifaa vingine vilikuwemo kwenye ghala hilo la Kinshasa ikiwa ni masaa kadhaa tangu Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo (CENI) ilipotangaza kupokea vifaa mbalimbali vya uchaguzi ikiwemo mashine za kupigia kura.

Kampeni za kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, zinaendelea baada ya kuanza rasmi Novemba 22, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa tarehe 23 mwezi Desemba.

Tume hiyo ya Uchaguzi ilisema kuwa imeorodhesha wapiga kura milioni 40 wanaotarajia kushiriki uchaguzi huo katika vituo vya kupigia kura 80,000 ambavyo vitakuwa na ‘mashine za kupigia kura” zaidi ya 100,000.

Kampeni zinaendelea wakati huu, kukiwa na mvutano mkubwa kuhusu suala la matumizi ya mashine za kupigia kura, pamoja na changamoto za kiusalama, mashariki mwa nchi hiyo. Wanasiasa wa upinzani, akiwemo mmoja wa wagombea wa upinzani, Martin Fayulu anaona kwamba mashine hizo haziaminiki na zitatumiwa kwaajili ya kuiba kura.