Katibu wa Mufti Zanzibar Khalid Ali Mfaume amewataka Maimamu wa Miskiti Unguja na Pemba kuomba dua na kuleta kunuti kila baada ya swala ili kujikinga na maradhi ya kupumua .

Ameyasema hayo huko Ofisini kwake Mazizini  Mjini Unguja  wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali kuhusiana na kuchukua tahadhari juu ya maradhi ya kuambukiza.

Amesema Ofisi ya Mufti ina wajibu wa kusimamia  na kufuatilia misikiti yote pamoja na madrasa kuhakikisha kuwa utaratibu wa kujikinga na maradhi unafuatwa hivyo ni wajibu wao maimamu na walimu wa madrasa kuweka vifaa muhimu vinavyotumika kujikinga ikiwemo maji, sabuni na vitakasa mikono.

 Katibu amefahamisha kuwa waislamu wakifikwa na mitihani wanatakiwa kurudi kwa Mwenyezi Mungu na kumuomba msamaha hivyo hakuna budi kufanya hivyo kwa kila muumini kwa lengo la kuchukua tahadhari ya kujikinga na kujiepusha na maradhi hayo Unguja na Pemba.

“Turudi kwa Allah (SW) na kuomba kwa maimamu wa misikiti yote Unguja na Pemba ili atuepushe na maradhi mabaya yanayoambukiza hasa maradhi ya kupumua ambayo nchi nyingi imekumbwa na janga hili,” alisema Katibu wa Mufti.

Aidha amewatahadharisha waumini kuchukua tahadhari wanapokuwa katika mikusanyiko mbalimbali ikiwemo maziko, mihadhara ili kujikinga pamoja na  kupeana nafasi baina ya mtu na mtu ili kuepusha uwezekano wa maambukizi.

Akizungumzia suala la ibada Katibu Khalid amewataka maimamu kuwasimamia waadhini misikitini kufuata wakati ili kwenda sambamba kiibada kwani kuna baadhi ya maimu wanaadhini kabla ya mda jambo ambalo linapelekea kutochunga ibada zao.

Aidha amewataka  maimamu kuwahimiza wanaochinja kufuata taratibu za kuchinja ili kuwaepusha waumini kula nyama ambazo hazina uhalali  kwani kuna baadhi ya watu wanakwenda kinyume na taratibu za kuchinja.

Hata hivyo Katibu huyo amefahamisha kuwa kwa sasa hakuna dua maalum  isipokuwa kwa hatua ya mwanzo waumini watumie dua mbalimbali ili kumuomba Mungu awakinge na   maradhi mbalimbali hasa ya kupumua.

Story Na Rahma Khamis  Maelezo-Zanzibar.